KAULI ya Mwenyekiti wa Klabu ya Simba, Ismail Rage (Pichani), kudai hawezi kujenga uwanja wa klabu hiyo ndani ya miaka mitatu, kwani hata serikali ilipita miaka 50 hadi kujenga Uwanja wa Taifa, imepingwa na baadhi ya wanachama.
Wanachama hao, wamemtaka mwenyekiti huyo kuacha kujitetea juu ya udhaifu alionao katika klabu hiyo, bali awajibike.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, mmoja wa wanachama wa Simba, Hassan Msumari, alisema ni ubabaishaji unaofanywa na mwenyekiti huyo kujifananisha na serikali ya nchi kujenga uwanja mmoja ndani ya miaka 50, kitu ambacho kwa upande wake kimekuwa kigumu kufanikiwa angalau kuanza kujenga uwanja wa klabu hiyo.
“Serikali kwa kipindi cha miaka 50, imefanya mambo mengi makubwa, hususan katika suala zima la maendeleo ikiwemo ujenzi wa shule na rasilimali nyingine nyingi ambazo wananchi hivi sasa wananufaika nazo, hivyo Rage asitumie mwanya wa Uwanja wa Taifa kuficha udhaifu wake,” alisema.
Vile vile alisema anashangaa kuona mwenyekiti huyo anategemea zaidi michango ya fedha za wanachama kuendesha klabu, kitu ambacho hakiwezekani, kwani wanachama hawafikii hata milioni tano ukilinganisha na kodi ya serikali ya simu-kadi ambayo imezingatia idadi ya Watanzania.
Aidha Msumari alisema Rage amekuwa akitumia zaidi mawazo yake katika uamuzi wa masuala ya klabu bila kushirikisha wanachama, jambo ambalo si sahihi.
Rage alitoa kauli hiyo Jumamosi iliyopita wakati akijibu moja ya maswali ya wanachama waliotaka kujua hatma ya ujenzi wa uwanja wa klabu hiyo, kama ambavyo mwenyekiti huyo alivyokuwa ametoa ahadi mwaka juzi.