MSANII wa muziki wa kizazi kipya nchini, Seif Shabani ‘Matonya’ (Pichani) yupo katika hatua za mwisho za uandaaji wa kibao chake kipya kinachokwenda kwa jina la ‘Tonya wa Leo’.
Matonya, kwa sasa anatamba na kibao chake cha ‘Zilipendwa’ ambacho kinafanya vizuri katika vituo mbalimbali vya redio na televisheni kutokana na maudhui yaliyomo ndani yake.
Aliwaomba mashabiki wake, wakae mkao wa kula kwa ajili ya kuipokea kazi hiyo ambayo anaamini itafanya vizuri.
“Mashabiki wangu wananijua kwamba nipo kamili na huwa sitoi vitu ambavyo havijakamilika, naomba wakae mkao wa kula kwa ajili ya kuipokea kazi hiyo ambayo itakuja pamoja na video yake,” alisema.
Mbali na kazi hizo, mkali huyo alishawahi kutamba na vibao vyake kama, ‘Taxi Bubu’, ‘Violeth’ na vinginevyo ambavyo vilimtambulisha katika tasnia ya muziki wa bongo fleva.