Baada mchezo usiyoridhisha
katika kipindi cha kwanza, mshambulizi wa Barcelona Lionel Messi
alijifurukuta na kufunga bao la ushindi la Argentina dhidi ya
Bosnia-Herzegovina katika mechi yao ya ufunguzi wa kampeini ya kombe la
dunia linaloendelea huko Brazil.
Bosnia-Herzegovina, ilikuwa imejifunga yenyewe kunako dakika ya tatu ya kipindi cha kwanza kupitia kwa Sead Kolasinac.
Limbukeni hao wa fainali ya kombe la dunia hawakukubali kushindwa bila ya kuonyesha ushindani wao .
Mchezaji wao wa akiba, Vedad Ibisevic, aliipatia timu yake matumaini katika dakika ya 85, alipofunga bao la kwanza la Bosnia, katika kombe la dunia .
Argentina inayojivunia vipaji kamilifu katika kila idara ililazimika kumwacha nje mshambulizi wa Napoli, Gonzalo Higuain, akiuguza jeraha.
Izet Hajrovic alikaribia kuisawazishia Bosnia katika dakika ya 13, lakini mlinda lango wa Argentina, Sergio Romero alizuia jaribio hilo la Hajrovic.
Licha ya kuanza kampeni yao vibaya, timu ya Bosnia ilionyesha mchezo mzuri haswa katika safu ya ulinzi ila tu ilihitaji kutia bidii katika mashambulizi yao.
Argentina, Maxi Rodriguez, alipiga mkwaju ambao ulipaa juu ya lango kabla ya muda wa mapumziko.
Jaribio lake Javier Mascherano pia lilizuiwa na mlinda lango wa Bosnia.
Hata hivyo, timu ya Argentina ilishikilia uongozi na kutwaa ushindi.