Kwa matokeo hayo katika Kundi C, Ivory Coast
imefikisha pointi 13 ambazo haziwezi kufikiwa na timu nyingine katika
kundi hilo hivyo imeingia raundi ya tatu, wakati Morocco ipo nafasi ya
pili ikiwa na pointi nane wakati Tanzania ipo nafasi ya tatu ikiwa na
pointi sita na Gambia inashika mkia ikiwa na pointi moja.
Taifa Stars imebakisha mechi moja dhidi ya Gambia
itakayochezwa huko Banjul mwezi Septemba, pia Ivory Coast imebakisha
mechi dhidi ya Morocco itakayochezwa huko Abidjan.
Katika mechi jana, Taifa Stars ilipata bao la
kuongoza katika dakika ya 1 ambalo lilifungwa na Amri Kiemba kwa shuti
kali la karibu akiwa ndani ya 18 baada ya mabeki wa Ivory Coast kusuasua
kuondoa mpira wa tik taka uliopigwa na Mbwana Samatta.
Timu ziliendelea kushambuliana kwa zamu, ambapo
dakika ya 13, Ivory Coast walisawazisha bao kupitia kwa mshambuliaji wao
Lacina Traore ambaye alimalizia kwa mguu krosi ya Gervinho ambaye kabla
ya kumpa mfungaji alimlamba chenga beki wa Stars, Erasto Nyoni.
Dakika ya 23, Ivory Coast walipata bao la pili
ambalo lilifungwa na Yaya Toure kwa mkwaju wa adhabu ndogo akiwa nje ya
18 baada ya Solomon Kalou kufanyiwa madhambi Frank Dumayo.
Baada ya kufungwa bao hilo, Taifa Stars haikukata
tamaa kwani iliendelea kupeleka mashambulizi katika lango la Ivory
Coast, ambapo ilipata bao la kusawazisha katika dakika 34 mfungaji akiwa
Ulimwengu ambaye aliunganisha vizuri krosi ya Shomari ambaye alipanda
kwa kasi akitokea winga ya kushoto.
Mpira ukiwa unaelekea mapumziko, Ivory Coast
ilipata penalti katika dakika ya 42 ambayo iliwekwa wavuni na Yaya Toure
na hivyo Ivory Coast kwenda mapumziko ikiongoza 3-2.
Penalti hiyo ilitokea baada ya Nyoni kumsukuma
Gervinho katika eneo la hatari na hivyo mwamuzi Mehdi Abid kuamuru
penalti. Kitendo hicho kilimuudhi kocha wa Stars, Kim Poulsen.
Kipindi cha pili Ivory Coast walianza tena kwa
kasi na katika dakika ya 49 Gervinho aliwazidi mbio mabeki wa Stars na
kumpa pande Kalou ambaye alipiga mkwaju uliogonga mwamba wa juu wa Stars
na kurudi uwanjani.
Katika mechi hiyo, wachezaji wa Stars waliisumbua
sana Ivory Coast, lakini timu ya Ivory Coast inayoundwa na wachezaji
wanaocheza soka la kulipwa katika klabu za Ulaya walikuwa walitumia
uzoefu zaidi.
Dakika ya 70 kipa wa Ivory Coast, Barry Boubacar
alifanya kazi ya ziada kupangua shuti kali la mpira wa adhabu ambalo
lilipigwa na Samatta.