come

come
Tuletee habari za kijamii, michezo na burudani, email kabumbu1935@gmail.com

YANGA KUJIFUA TENA ULAYA

MABINGWA wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara, Yanga wamesema endapo serikali ya Tanzania itaendeleza msimamo wake wa kutoruhusu timu za Tanzania kushiriki katika michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (Kombe la Kagame), wataipeleka timu yao barani Ulaya kuweka kambi maalum kwa ajili ya kuiimarisha.


Juni Mosi mwaka huu akijibu hoja za wabunge walizozitoa katika kuchangia bajeti ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Bungeni mjini Dodoma, Waziri wa Wizara hiyo, Bernard Membe alikataza timu za Tanzania kwenda kushiriki Kombe la Kagame kwa kuwa hali ya usalama kwenye Jimbo Darfur, ambalo ni moja ya vituo vilivyopangwa kufanyika kwa michuano hiyo mwaka huu, ni ya wasiwasi na kwamba watu wanaokwenda huko wanapokewa na vikosi vya magari ya kujeshi na huvishwa nguo ambazo hazipenyezi risasi.

Akizungumza na mtandao huu jijini Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu wa Yanga, Lawrence Mwalusako alisema kuwa wanasubiri tamko la mwisho la serikali kujua kama kuna uwezekano wa wao kushiriki katika michuano hiyo mwaka huu.

Alisema kuwa klabu yao iko katika mipango ya kuimarisha kikosi chake kwa ajili ya msimu ujao wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara na mashindano ya kimataifa na kwamba wana mpango wa kuweka kambi nje ya mipaka ya Tanzania kama walivyofanya kabla ya kuanza kwa mzunguko wa pili wa ligi msimu uliopita walipoweka kambi ya wiki mbili katika mji wa Antalya, Uturuki.
“Mipango yetu ya sasa ni kufanya usajili makini ili kuimarisha kikosi.

Endapo serikali itasimamia ilichokisema hapo awali kwamba tusishiriki Kombe la Kagame, basi tutaangalia mahali pa kupeleka timu yetu ikajifue vizuri,” alisema Mwalusako.

“Tumepanga kuipeleka nje ya nchi na tunachosubiri kwa sasa ni mapendekezo ya kocha (Mholanzi Ernie Brandts) anataka timu iende nchi gani ya Ulaya na hata mabara mengine,” aliongeza Mwalusako.

Aidha, Katibu Mkuu huyo alisema kuwa kikosi chao kinachowakosa nyota kadhaa wakiwamo viungo Frank Domayo na Haruna Niyonzima na mabeki Nadir Haroub ‘Cannavaro na Kelvin Yondan ambao wako kwenye timu zao za taifa, kinaendelea na mazoezi kwenye Uwanja wa Shule ya Sekondari Loyola uliopo Mabibo jijini Dar es Salaam chini na Brandts na msaidizi wake, Felix Minziro. 

Michuano ya Kombe la Kagame mwaka huu iliyopangwa kuanza Juni 18 na kumalizika Julai 2, imepangwa kucheza katika mji wa Kadugli uliopo Kordofan Kusini na mji wa Alfashery uliopo Darfur Kaskazini, eneo ambalo limezua hofu kutokana na kukumbwa na vita vya wenyeji kwa muda mrefu.

Mabingwa watetezi Yanga, Simba na Super Falcon ya Zanzibar ni miongoni mwa timu 13 zinazotakiwa kushiriki michuano hiyo inayodhaminiwa na Rais wa Rwanda, Paul Kagame.