come

come
Tuletee habari za kijamii, michezo na burudani, email kabumbu1935@gmail.com

MAKALA: HAYA NDIO MAPUNGUFU YA IVO MAPUNDA, SIMBA MSIMHUKUMU.

Na Fikiri Salum.

ZIMEBAKI siku tatu kabla ya rais wa kwanza mweusi wa Afrika Kusini Nelson Mandela hajafikishwa kwenye nyumba yake ya milele, dunia nzima imehamia kusini mwa Afrika kushiriki tukio la aina yake ambalo halijapata kutokea ama halitatokea tena.

Viongozi wote duniani wameudhuria katika msiba wa mwokozi huyo wa taifa la Afrika Kusini, kikubwa kwa Nelson Mandela alikubali kutumikia kifungo cha maisha ili kuwakomboa watu weusi waliokuwa katika mateso ya ubaguzi wa rangi chini ya makaburu.

Nirejee kwenye mada husika, Wekundu wa Msimbazi Simba wako mbioni kumalizana na kipa wa timu ya Gor Mahia pamoja na Taifa Stars Ivo Mapunda (Pichani akiokoa shuti kali golini kwake) ambaye aliwahi kuzichezea Tanzania Prisons ya Mbeya, Moro United ya Morogoro na Yanga.

Simba imetangaza kumpa mkataba wa miaka miwili kipa huyo ambaye aling'ara katika michuano ya Chalenji inayofikia kilele leo nchini Kenya ambapo miamba Kenya na Sudan itakutana katika mchezo wa fainali.


Mapunda alionyesha umahiri wake katika mchezo wa robo fainali ambapo aliiwezesha Kill Stars kuingia nusu fainali baada ya kuzuia michomo ya penalti mbili za Uganda.

Umahiri na uzoefu wa kipa huyo mwenye umri wa miaka 29 uliweza kuwashangaza wengi, viongozi wa klabu ya Simba ambao wapo nchini Kenya kufuatilia fainali hizo waliamua kumsainisha kipa huyo ambaye kwa sasa ndiye Tanzania One badala ya Juma Kaseja aliyetemwa katika kikosi hicho kwa sababu kuwa amekosa timu.

Licha ya kusajiliwa na Yanga, Kaseja bado hajaweza kumshawishi kocha wa Stars Kim Poulsen kwa sababu hajaonekana akiitumikia timu yake mpya ya Yanga, Tayari Simba wameanza kuwa na furaha kutokana na usajili huo wa Ivo Mapunda.

Imekuwa jambo la kawaida na furaha kwa vilabu vikongwe vya Simba na Yanga vinaposajili wachezaji gumzo, lakinoi baadaye hujikuta wakishindwa kujizuia pindi wanapofanya vibaya lawama zote huzielekeza kwa wachezaji hasa mpya aliyesajiliwa.

Imekuwa hivyo kwa timu hizi ambazo zimeozea kuua viwango vya wachezaji wake hadharani, Yanga ilianza kushangilia pale ilipomsajili kipa wa zamani wa Simba Ally Mustapha 'Barthez'.

Lakini katika mchezo wake wa kwanza wa ligi kuu ya Vodacom Tanzania bara dhidi ya Simba na kushuhudia sare ya mshangao ya 3-3 lawama nyingi zilielekezwa kwa kipa wake Barthez ambaye anadaiwa alicheza chini ya kiwango.

Baadaye lawama hizo zilielekea upande wa Simba ambao walimshutumu waziwazi kipa wao Abel Dhaira, katika mechi za ligi zilizofuatia timu zote hizo ziliwatosa makipa wake waliocheza mechi ilizowakutanisha.

Yanga iliamua kumpumzisha kipa wake Barthez na nafasi yake ilichukuliwa na Deogratus Munishi 'Dida', wakati Simba nayo iliamua kumweka benchi Dhaira na mikoba alikabidhiwa chipukizi Abou Hashimu.

Baada ya mzunguko wa kwanza kumalizika, Yanga ilitangaza kumsajili kipa mpya Juma Kaseja ambaye aliachwa na klabu yake ya zamani ya Simba, Simba nao waliamua kumpa mkataba wa miezi sita Yaw Berko ambaye naye aliwahi kuitumikia Yanga.

Simba pia haikuridhishwa na usajili wa Berko na ndipo inapofanya kila liwezalo impe mkataba wa miaka miwili kipa mzoefu katika ukanda huu wa Afrika mashariki Ivo Mapunda ambaye amecheza vizuri katika michuano ya Chalenji.

Ivo bado hajasaini rasmi Simba ila muda wowote anaweza kumwaga wino na ataitumikia Simba katika mechi ya Nani Mtani Jembe itakayofanyika Desemba 21 mwaka huu kwenye uwanja wa Taifa.

Lakini nawakumbusha kitu kimoja watu wa Simba hasa mashabiki wao ambao wana kawaida ya kung'oa viti pindi timu yao inapofungwa, Ivo Mapunda ana tatizo moja tu ambalo linaweza kuigharimu Simba, ila nawasihi wasijaribu kumhukumu.

Kipa huyo mwenye umbo la kimichezo na anayeaminiwa na kocha yeyote yule ni mzuri awapo golini, na sifa yake kubwa kucheza mipira ya krosi, kona pamoja na faulo, lakini kosa lake kubwa ambalo si rahisi kuvumilika na lile la kutema mipira hovyo kwenye eneo la hatari.

Tatizo hilo pia ndilo lililoigharimu Kill Stars ilipocheza na Harambee Stars na kukubali kipigo cha bao 1-0, vijana wa Kenya walijipatia goli lao baada ya shuti kali lililopigwa na Criffod Mihesu ambapo Ivo Mapunda badala ya kuupangua mpira huo alitaka kuudaka na kuutema.

Mbaya zaidi alimtemea mfungaji ambaye hakupata shida aliuweka kimiani, hilo ndio tatizo la Ivo Mapunda ambaye leo hii mashabiki wa Simba wanashangilia kutua msimbazi kipa huyo lakini wasije kumwadhibu pale atakapotema shuti la Hamisi Kiiza na Mrisho Ngasa akafunga kirahisi na kuzusha songombingo lingine.

Ivo Mapunda anafahamika vizuri katika ligi kuu ya bara, ni rahisi wachezaji wanaomfahamu kumtungua, pia wanalijua tatizo lake la kutematema ambalo ndilo lililochangia kumuondoa katika ligi kuu ya bara wakati alipokuwa akiitumikia klabu ya Yanga na timu ya taifa, Taifa Stars.

Mapunda alipata kuichezea Taifa Stars kwa mafanikio enzi za Mbrazil Marcio Maximo lakini wanaharakati wa masuala ya soka walishinikiza kipa hiyo aondolewe Stars kwa madai uwezo wake ni mdogo mbele ya Juma Kaseja aliyewekewa ngumu na Maximo akidai ni mtovu wa nidhamu.

Enzi hizo Kaseja alikuwa akichezea Simba, lakini TFF ilimuondoa Maximo na ndio ukawa mwisho wa Mapunda kuitwa timu ya taifa, Taifa Stars mpaka pale Kim Poulsen alipofanya hivyo tena mwaka huu ikiwa Ivo ni mchezaji wa Gor Mahia ya Kenya.

Mwandishi wa makala hii anapatikana kwa namba 0755 522216, Toa maoni yako.