come

come
Tuletee habari za kijamii, michezo na burudani, email kabumbu1935@gmail.com

SHADRACK NSAJIGWA AANIKA MAISHA YAKE KITABUNI

Nahodha wa zamani wa Yanga anayeifundisha hivi sasa timu ya Lipuli ya Iringa, Shadrack Nsajigwa “Fuso” (Pichani) amepanga kutoa kitabu kinachozungumzia historia ya maisha yake.


Akizungumza mjini hapa, Nsajigwa alisema historia yake atakayoizungumzia kwenye kitabu hicho inajumuisha maisha yake ya utoto, shule, soka kama mchezaji mpaka kuwa kocha.

“Nipo katika maandalizi ya kutoa kitabu changu kitakachozungumzia maisha yangu tangu utoto, shule, soka na mpaka nimekuwa kocha,” alisema Nsajigwa na kuongeza:

“Ni historia ya kuvutia kwa kweli ambayo watu watapata fursa nzuri ya kumjua Nsajigwa, wapi alipotokea mpaka kuja kufahamika katika ulimwengu wa soka,” alisema Nsajigwa.

Wakati huohuo, Nsajigwa alisema anaamini Lipuli itafanya vizuri katika Ligi Daraja la Kwanza inayotarajiwa kuanza mapema mwezi ujao.

“Nina wachezaji wenye uzoefu kama Godfrey Bonny, Benjamin Haule, Paul Kabange na Sammy Kessy ambao naamini kwa kushirikiana na chipukizi wengi timu itafanya vizuri na Mungu akijalia Lipuli itarudi Ligi Kuu,” alisema Nsajigwa.

Nsajigwa ambaye pia aliwahi kuwa nahodha wa timu ya Taifa ‘Taifa Stars’ kwa miaka kadhaa ameibukia kwenye ukocha baada ya kumaliza mkataba wake katika klabu ya Yanga.