Na Fikiri Salum.
HUENDA sasa kikosi cha Simba kinachonolewa na Mcroatia Zdravko Lugarasic kikakumbana na kipigo kikubwa tena cha kulipiza kisasi endapo tu watashindwa kuweka ushindani mkubwa dhidi ya mahasimu wao wakubwa nchini Yanga watakapokutana katika mechi ya Ngao ya Hisani maarufu Mtani Jembe iliyoandaliwa na wadhamini wao wakuu Kilimanjaro Primier Lager.
Tayari Yanga imeanza kutambia kikosi chake na kudai ni cha kushiriki ligi ya mabingwa Afrika na kinatarajia kuiteketeza kabisa Simba kwenye uwanja wa Taifa siku hiyo ya Jumamosi ya tarehe 21 mwezi huu kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Katika mchezo huo Yanga inatarajia kuwatumia nyota wake wote wanaong'ara wakiongozwa na kipa mashuhuri nchini Juma Kaseja, pia watakuwepo nyota wengine kama vile Haruna Niyonzima, Mrisho Ngasa, Hamisi Kiiza, Didier Kavumbagu, Hassan Dilunga, Athuman Idd 'Chuji', Kelvin Yondani, Nadir Haroub 'Cannavaro', Simon Msuva na Mbuyu Twite na wengineo.
Taarifa zilizopatikana kutoka Jangwani zinadai kuwa Yanga imepanga kuishushia kipigo kikubwa Simba ili waendeleze mgogoro wao wa kupinduana, mbali na kupata ushindi huo pia wanataka kuionyesha Simba kuwa wao wamejipanga msimu huu kutwaa ubingwa wa bara pamoja na kufika hatua za mbali katika ligi ya mabingwa Afrika.
Timu hizo zilikutana katika mchezo wa ligi kuu mzunguko wa kwanza ambapo zilitoshana nguvu kwa kufungana mabao 3-3, Yanga ilikuwa mbele hadi mapumziko ikiwa na mabao hayo matatu lakini ilijikuta ikiruhusu magoli matatu katika kipindi cha pili na kufanya matokeo yasomemeke kuwa 3-3.
Hivyo wanataka kudhihirisha kuwa wanao uwezo wa kuifunga Simba tena magoli mengi, lakini kikosi cha Wekundu wa Msimbazi kimeanza mazoezi makali kujiandaa na mchezo huo wa kukata na shoka, Simba imeamua kuwasajili waliokuwa makipa wa zamani wa Yanga Ivo Mapunda na Yaw Berko ili kucheza katika mchezo huo unaosubiriwa kwa hamu na wapenzi wa soka hapa nchini.