KIUNGO wa Yanga na timu ya Taifa ya Rwanda ‘Amavubi’, Haruna Niyonzima amesema straika Birori Dady aliyeivurugia nchi yake kucheza hatua ya makundi kufuzu Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) alikuwa na ajenda ya siri.
Rwanda ilikuwa imeshafuzu kucheza hatua ya makundi ikiwekwa Kundi A sambamba na Nigeria, Afrika Kusini na Sudan lakini Agosti 18, mwaka huu Shirikisho la Soka Afrika (Caf) liliiondoa timu hiyo kwa kumchezesha Birori mwenye pasipoti mbili.
Niyonzima alisema “Unajua mimi hainiingii akilini kabisa kwamba mtu mzima na akili zake anaweza kufanya siri kitu kikubwa kama kuwa na pasipoti mbili na anajua kabisa kufanya hivyo ni kinyume na kanuni.
“Sisi tumepambana na tumefungiwa kwa uzembe wake, mimi naona amefanya makusudi tu ili atuvuruge na amefanikiwa hakuwa na nia nzuri na sisi. Sasa sina hata hamu ya kuichezea timu ya Taifa kwa sababu yake.”
Birori alibainika kuwa na pasipoti mbili ambapo ya kwanza aliyopewa Rwanda ina jina la Daddy Birori inaonyesha amezaliwa Desemba 12, 1986 lakini ya pili iliyotolewa DR Congo ina jina la Etekiama Agil Taddy inaonyesha amezaliwa Desemba 13, 1990.
Utata wa Birori uliibuliwa na Congo waliohoji uhalali wa straika huyo kuichezea Rwanda akiwa na pasipoti mbili lakini hata Libya pia walihoji uhalali wa mchezaji huyo ambaye aliwafunga mabao matatu ‘hat trick’ Mei 31, mwaka huu katika mechi ya mtoano Uwanja wa Nyamirambo, Kigali.
Caf ilitumia kanuni ya 41 ya michuano ya Kombe la Afrika ibara ya 82 na 83.1 kumfungia Birori kwa kosa hilo.
Chanzo Mwanaspoti