Rais wa Afrika Kusini Jacob Zuma
amefutilia mbali ziara yake ya kwenda Musumbiji baada ya kumtembelea
hospitalini aliyekuwa Rais wa Afrika Kusini, Nelson Mandela. Rais Zuma
amesema kuwa Bwana Mandela yuko katika hali mbali ya afya.
Msemaji wa Zuma Mac Maharaj amesema kuwa hali yake imedorora zaidi katika saa 48 zilizopita.
Mandela ambaye, ni rais wa kwanza mweusi wa Afrika Kusini, amelazwa hospitalini tangu tarehe 8 mwezi Juni akiugua maradhi ya mapafu.
Madaktari wanasemekana kufanya kila wawezalo kuhakikisha kuwa Mandela anapona.
Vikundi vya watu wenye huzuni mkubwa kuhusu hali ya afya ya Mandela, walikusanyika nje ya hospitali alikolazwa, wakiwa na ujumbe wa ugua pole kwa Mandela
Wadadisi wanasema kuwa wananchi wa Afrika Kusini wanaonekana kuwa tayari kwa habari zozote sasa kuhusu hali ya Mandela.
"tutasikitika sana ikiwa tutapata habari za kifo chake, lakini pia tutakuwa tunasherehekea maisha yake. Amefanya mambo mengi zaidi kwa nchi yetu,'' alisema kijana John Ndlovu, mwenye umri wa miaka 25.
Zuma alitarajiwa kuhudhuria mkutano wa marais nchini Msumbiji, hii leo lakini akaamua kuakhirisha safari yake.
Taarifa kutoka kwa ofisi yake ilisema kuwa anaendelea kuwapongeza wananchi wa Afrika Kusini wanaoendelea kuiombea familia ya Madiba.
Uamuzi wa Rais Zuma kufutilia mbali ziara yake ambako alitarajiwa kuhudhuria mkutano wa kikanda kuhusu uekezaji anaonyesha wazi kuwa hali ya Mandela inaendelea kuzorota zaidi kulingana na mwandishi wa BBC mjini Johannesburg Mike Wooldridge.