Kanuni inayozitaka klabu za ligi kuu kusajili nyota
wa kigeni wasiozidi watatu inaonekana kuuchanganya uongozi wa Azam baada
ya jana kusema kwamba utakaa kujadili kufyeka nyota wake wa kigeni.
Azam ina wachezaji watano wa kigeni ambao ni raia wa Ivory Coast, Kipre
Bolou na Kipre Tchetche ambaye ni mfungaji bora wa msimu uliopita,
Wakenya Joackins Atudo na Humphrey Mieno na Mganda Brian Umony.
Akizungumza jana jijini Dar es Salaam jana, Meneja wa Azam,
Patrick Kahemele alisema bodi ya 'Wanalambalamba' itakutana kujadili
suala hilo.
"Suala hilo ni zito, siwezi kulitolea maelezo kwa sasa (jana). Bodi ya
klabu itakaa kulijadili ili tujue wachezaji wawili watakaopunguzwa na
hatua nyingine za kuchukua," alisema Kahemele.
Mapema jana, Mwenyekiti wa Kamati ya Ligi ya Shirikisho la Soka (TFF),
Wallace Karia aliliambia gazeti hili jijini Dar es Salaam kuwa kamati za
usajili za klabu zinazoshiriki Ligi Kuu ya Tanzania Bara zinapaswa
kuzingatia kanuni katika kusajili wachezaji.
TFF kupitia kwa afisa habari wake, Boniface Wambura imeshaeleza kuwa
kuanzia msimu wa 2013/14, kila klabu inayoshiriki Ligi Kuu ya Tanzania
Bara itatakiwa kuwa na wachezaji wa kigeni wasiozidi watatu ili
kutekeleza walichokubaliana na klabu katika mkutano uliofanyika jijini
Dar es Salaam 2010 kupitisha Azimio la Bagamoyo ambalo linataka kila
klabu kuwa na nyota wa kigeni wasiozidi watatu ili kuwapa nafasi zaidi
ya kucheza wachezaji wazawa.
Klabu za Simba na Yanga pia ni waathirika wakubwa wa maamuzi hayo kwani
msimu uliopita zilisajili wachezaji wa kigeni zaidi ya watatu.
Msimu uliopita ambao klabu zilikuwa zinaruhusiwa kuwa na wachezaji wa
kigeni wasiozidi watano, Yanga ilikuwa na Yaw Berko wa Ghana, Haruna
Niyonzima 'Fabregas' na Mbuyu Twite (Rwanda), Didier Kavumbagu (Burundi)
na Mganda Hamis Kiiza.
Simba ilikuwa na Waganda Mussa Mude na Emmanuel Okwi ambaye baadaye
aliuzwa katika klabu ya Etoile du Sahel ya Tunisia, Pascal Ochieng
(Kenya), Komalbil Keita (Mali), Daniel Akuffor (Ghana) na Mzambia Felix
Sunzu.