Kiemba, ambaye alifunga goli pekee la Taifa Stars katika mechi waliyolala 2-1 dhidi ya Morocco (Simba wa Atlas) ugenini jijini Marrakech, Morocco Juni 8 na kisha kufunga goli la kwanza katika mechi ya Stars dhidi Ivory Coast jijini Dar es Salaam Juni 16, alinyakuwa tuzo hiyo akiwabwaga Kipre Tchetche wa Azam, ambaye Mfungaji Bora wa Ligi Kuu ya Bara msimu uliopita, Haruna Niyonzima 'Fabregas' na Didier Kavumbagu (Yanga) na Paul Nonga wa JKT Oljoro.
Kiungo Salum Aboubakar 'Sure Boy' wa Azam aliwashinda Shomari Kapombe, Shukuru Salum, Hassan Dilunga na Issa Rashid na kutwaa tuzo ya Mchezaji Bora Chipukizi huku kipa Hussein Sharif wa Mtibwa Sugar akinyakuwa tuzo ya Kipa Bora wa Mwaka akiwafunika Juma Kaseja (Simba) na Mwadini Alli wa Azam.
Kocha wa Mtibwa na nahodha wa zamani wa Taifa Stars, Mecky Mexime alitwaa tuzo ya Kocha Bora wa Mwaka baada ya kuwazidi kura makocha Abdallah Kibaden 'King' (Kagera Sugar), Boniface Mkwasa (Ruvu Shooting) na Jumanne Chale wa Tanzania Prisons.
Katibu Mkuu wa SPUTANZA, Said George alisema kuwa majina ya wachezaji waliopigiwa kura na manahodha na makocha wa timu zote 14, waliyapata katika idara ya takwimu ya Shirikisho la Soka (TFF) na kwamba vigezo vilivyotumika kuwapata ni nidhamu, uwezo wa uwanjani na kuwa pamoja na timu mwanzo-mwisho wa msimu wa 2012/13 wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara.
VITUKO:
Kituko cha kwanza kilikuwa kutozwa viingilio watu waliojitokeza kushuhudia tuzo hizo. Kiingilio kilikuwa Sh.10,000 na Sh.50,000 kwa waliokaa eneo maalum (VIP). "Nimechelewa kidogo kuingia ukumbini kwa sababu nilizuiwa pale mlangoni ikabidi nitoe Sh.10,000 ya kiingilio," alisema Sure Boy katika mahojiano na baada ya kushinda tuzo ya Mchezaji Bora Chipukizi.
Kituko cha pili kilijitokeza pale mshehereshaji (jina linahifadhiwa) alipokuwa akitaja majina ya makipa waliokuwa wakiwania tuzo ya Kipa Bora wa Mwaka. "Mabibi na mabwana katika kipengele hiki wanachuana Juma K. Juma wa Simba, Mwadini Alli wa Mtibwa na Hussein Sharif kutoka Azam." Ukweli ni kwamba Sharif ni kipa wa Mtibwa na Mwadini ni kipa wa Azam.
Baada ya kusomwa kwa orodha hiyo ya makipa, mmoja wa viongozi wa waandaji wa tuzo hizo (jina linahifadhiwa), aliibua 'kioja' kingine wakati alipokuwa anajiandaa kutaja mshindi wa tuzo hiyo.
"Mchezaji Bora wa Mwaka ni.... " alisema huku akisita kumalizia baada ya kubaini kuwa karatasi aliyokuwa amepewa, ilikuwa ni ya kutaja Mchezaji Bora wa Mwaka badala ya Kipa Bora wa Mwaka.
Kukosewa kwa jina la kiungo Niyonzima wa Yanga lilikuwa tukio la nne. Mshereheshaji alisikika akisema: Wanaowania tuzo ya Mchezaji Bora wa Mwaka ni Amri Kiemba kutoka Simba, Haruna Moshi Niyonzima wa Yanga..." Hakuna mchezaji wa Yanga anayeitwa Haruna Moshi Niyonzima bali kuna Haruna Niyonzima ambaye pia ni kiungo wa timu ya taifa ya Rwanda (Amavubi).
Jambo jingine la kushangaza katika tuzo ni majina ya wawaniatuzo kujulikana ukumbini licha ya tuzo hizo kutangazwa mara kadhaa kupitia vyombo vya habari.
Aidha, zawadi za washindi wa tuzo hizo hazikuwekwa wazi. "Wametukabidhi vikombe na kutuambia kwamba tuonane ofisini kwao jijini Dar es Salaam ili watupe zawadi lakini hatujui ni kiasi gani cha pesa," alisema Mexime katika mahojiano na gazeti hili baada ya kutwaa tuzo ya Kocha Bora wa Mwaka.