Cecafa ilitangaza mashindano hayo kufanyika nchini
Sudan baada ya kuhakikishiwa na Serikali ya Khartoum uwepo wa usalama
wa kutosha kwenye jimbo la Darfur, ambalo limekuwa kwenye mapigano kwa
muda mrefu.
Katibu mkuu wa Cecafa, Nicholous Musonye
alikaririwa akizitaka nchi zinazoshiriki kutokuwa na wasiwasi juu ya
usalama wa nchi hiyo kwa sasa na kusisitiza usalama umeimarishwa sehemu
zote.
“Tumehakikishiwa usalama na Serikali ya Sudan, kwa
hiyo nchi zote zinazoshiriki zisiwe na wasiwasi katika hilo,”
alikaririwa Musonye.
Akiongea bungeni jana jijini Dodoma, wakati wa
majumuisho ya michango ya wabunge waliojadili makadirio ya matumizi ya
bajeti ya wizara hiyo mwaka 2013/2014, Waziri wa Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Kimataifa,
Bernard Membe, alisema hakuna uhakika wa nchini Sudan.
“Wizara inachunguza na itatoa taarifa kuhusu hali
ya usalama Sudan na kuna uwezekano mkubwa wa kuzuia ushiriki wa timu za
Tanzania” alisema na kuongeza;
“Tutachunguza na inawezekana kabisa tukawataka
wasiende katika mashindano hayo kwani uwepo wao nchini Sudan unaweza
kuleta fedheha kwa taifa letu.”
Katika ufafanuzi wake Membe alishangazwa na uamuzi wa Cecafa kwa kuchagua mji wa Darfur kufanyika kwa mashindano hayo.
“Darful hakuna hoteli na hali ya usalama ni ya
wasiwasi kweli na hata watu wanaokwenda huko wanapokewa na vikosi vya
magari yasiyoingia risasi BPV (Bullet Proof Vehicles) na huvishwa nguo
zisizoingia risasi,” alisema.
“Nimeshangaa mipango hii ya kupeleka wachezaji wa
Tanzania bila kutafakari usalama wa vijana utakuwa katika hali gani,
sijui kwa nini walichagua sehemu hii kufanyika mashindano haya.”
Tanzania inawakilishwa na Yanga kama bingwa
mtetezi wa michuano hiyo na Simba kama bingwa wa bara msimu uliopita.
Simba iko Kundi A na timu za El-Merrekh (Sudan), APR (Rwanda) na Elman
(Somalia), wakati Yanga iko Kundi C sambamba na Express (Uganda), Ports
(Djibout) na Vital’O (Burundi).