BEKI wa kimataifa wa Tanzania na timu ya Simba, Shomari Kapombe anatarajiwa kuondoka nchini hivi karibuni kwenda nchini Uholanzi kwa ajili ya majaribio ya kucheza soka la kulipwa katika klabu ya FC Twente.
Kapombe mwanasoka bora wa mwaka huu amekuwa na
mafanikio makubwa tangu alipojiunga na Simba akitokea Polisi Morogoro
miaka mitatu iliyopita kwa kuisaidia Simba kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu.
Hivi sasa Kapombe anatarajiwa kwenda kufanya
majaribio katika klabu ya FC Twente, ambayo ilitwaa ubingwa wa Ligi Kuu
ya Uholanzi katika msimu wa 2009-10, pia ilifanikiwa kucheza hatua ya
makundi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya katika msimu huo.
Katika msimu uliopita FC Twente imemaliza katika
nafasi ya sita katika Ligi Kuu ya Uholanzi ikiwa na pointi 62, huku Ajax
wakiwa mabingwa kwa pointi 76.
Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Simba, Swed Nkwabi akizungumza
jana jijini Dar es Salaam alisema,”timu atakayokwenda kufanya majaribio
Kapombe huko nchini Uholanzi ni FC Twente, suala la ataondoka lini
kwenda kufanya majaribio tutawaambia safari itakapokuwa tayari.”
Akizungumza katika kipindi cha Spoti Leo
cha Radio One juzi, Mwenyekiti wa Simba, Ismail Aden Rage alisema
amekwishatoa kibali kwa Kapombe kuondoka nchini siku yoyote kuanzia sasa
kwa ajili ya kufanya majaribio nchini Uholanzi.
Alisema Kapombe alitakiwa kuondoka mapema kwa
ajili ya majaribio hayo, lakini mpaka hivi sasa amechelewa zaidi ya siku
saba kutokana na kuisubiri mechi ya Taifa Stsr dhidi ya Ivory Coast ya
kuwania kufuzu Fainali za Kombe la Dunia imalizike.
Katika mchezo huo wa kusaka kufuzu kushiriki
Fainali za Kombe la Dunia 2014, dhidi ya Ivory Coast, Kapombe alichangia
kupatikana kwa bao la pili la Taifa Stars lililofungwa na Thomas
Ulimwengu.
Akizungumzia safari hiyo ya kwenda kufanya
majaribio ya kucheza soka nchini Uholanzi, Kapombe alisema mimi
nimeambiwa kuhusu safari hiyo, lakini sijui ni timu gani ninayokwenda
kufanya nayo majaribio.”
“Sijui ni lini nitaondoka kwa sababu hivi sasa
mimi ni majeruhi, niliumia katika mchezo dhidi ya Ivory Coast na
nimetakiwa kukaa nje ya uwanja kwa muda wa wiki moja au mbili,”alisema
Kapombe.
Katika hatua nyingine, Mwenyekiti wa Simba, Ismail
Rage alitoa ushauri kwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kumruhusu
mchezaji huyo kwenda kwenye majaribio hayo kwani akifanikiwa itakuwa ni
faida kwa Taifa.