Timu ya Coastal Union ya Tanga keshokutwa Jumatano itawatambulisha rasmi
mbele ya mashabiki wachezaji wake wapya Haruna Moshi 'Boban' na Juma
Nyoso (Pichani) katika mechi ya kirafiki dhidi ya URA ya Uganda kwenye Uwanja wa
Mkwakwani, Tanga.
URA ambayo juzi iliifunga Simba magoli 2-1 na jana kutoka sare ya 2-2
dhidi ya Yanga kwenye kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam,
inaondoka leo kwenda Tanga tayari kwa ajili ya mechi hiyo.
Akizungumza jana, kocha wa Coastal Union, Hemed Moroco,
alisema kuwa pamoja na mchezo huo kuwa sehemu yao ya maandalizi ya kwa
ajili ya msimu ujao wa ligi kuu, pia watautumia kwa ajili ya
kuwatambulisha nyota wao wapya wakiwamo wakongwe hao waliowasajili
kutoka katika klabu ya Simba.
"Huu mchezo ni muhimu zaidi kwetu katika maandalizi, tumekuwa tukifanya
mazoezi kwa muda sasa kwa hiyo URA watakuwa kipimo kizuri kwetu... na
pia tutawatambulisha rasmi kwa mashabiki wachezaji wetu wapya...
mashabiki wamekuwa wakisoma tu kwenye vyombo vya habari kuhusu usajili
wetu lakini sasa watapata nafasi ya kuwaona wachezaji hao uwanjani,"
alisema Moroco.
Aidha, alisema kuwa watautumia mchezo huo kuangalia mapungufu ya timu
yao katika kipindi hiki wanachojiandaa kwa ajili ya msimu mpya.
Aliwataka mashabiki wa soka mkoani humo kujitokeza kwa wingi kuwaangalia
wachezaji wao na maandalizi yao kwa ajili ya msimu ujao wa ligi kuu
unaotarajiwa kuanza Agosti 24 mwaka huu.
Kwa upande wake nahodha wa URA, Joseph Owino ambaye amewahi kuzichezea
timu za Simba na Azam, alisema anaamini mechi dhidi ya Coastal Union
itakuwa mzuri na yenye upinzani kwa kuwa amesikia mabadiliko ya timu
hiyo.
Alisema kuwa ziara yao ya kuja nchini itawasaidia sana katika kukijenga
upya kikosi chao ambacho kimesajili wachezaji wengi vijana.