BENDI kongwe ya muziki wa dansi nchini, Msondo Ngoma, (Pichani) imeingia studio kurekodi nyimbo zake mpya zitakazokuwa katika albamu moja.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Msemaji wa bendi hiyo, Rajabu Mhamila 'Super D’, alisema kuwa bendi yake kwa sasa imeingia studio kukamilisha kurekodi nyimbo zao mpya.
Alizitaja nyimbo hizo kuwa ni ‘Suluhu’ uliotungwa na Shabani Dede, ‘Lipi Jema’ na ‘Baba Kibebe’ wa Eddo Sanga na ‘Nadhiri ya Mapenzi’ wa Juma Katundu.
Nyimbo nyingine ni ‘Momba Hakuna Urithi’ na ‘Machimbo’, nyimbo zote hizo zikikamilika zitawekwa kwenye albamu moja kwa ajili ya kuwapa raha mashabiki wao.
Super D aliongeza kuwa bendi hiyo ambayo ilikuwa imesitisha maonesho yake kwa ajili ya mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani sasa wanajipanga kwa ajili ya kufanya maonesho katika Sikukuu ya Idd el Fitr.
Bendi hiyo, Idd Mosi itatoa burudani katika ukumbi wa DDC Kariakoo wakati Idd Pili watakuwa TTC Chang’ombe na Idd Tatu watavuka bahari kuelekea visiwa vya karafuu na kufanya onesho lao Zanzibar.