KOCHA wa Manchester United, David Moyes
anakabiliwa na baa la majeruhi, baada ya Robin van Persie kuumia wakati
wakifungwa mabao 3-2 na Yokohama F-Marinos jana Japan.
Moyes alisema baada ya mechi hiyo kwamba
Wayne Rooney aliyeumia nyama za paja anaendelea vizuri na atajiunga na
timu mjini Manchester akiwa anatarajia mchezaji huyo mwenye umri wa
miaka 27 atacheza mechi ya kirafiki Stockholm Agosti 6.
Mwalimu huyo wa United ameendelea
kusistiza Rooney hauzwi lakini pia amesema Van Persie amepata maumivu.
"Tumepata wiki kadhaa za shaka,"alisema Moyes.
"Robin aliumia kipindi cha kwanza na hatukutaka kumpa nafasi zaidi uwanjani. Danny
Welbeck pia anahisi maumivu ya nyonga wakati anatembea na tunatakiwa
kuhakikisha wote wanakuwa sawa, hususan kutokana na mechi nyingi mbele
yetu.
"Bado tuna mechi chache za kucheza kabla ya kuanza kwa msimu tutakaporudi nyumbani. Kama tunavyofahamu,
Wayne anakuja. Ameanza mazoezi mepesi ya kukimbia na taarifa nilizopata
kutoka watu wetu wa tiba ni kwamba anaendelea vizuri. Ni matumaini
mambo yatakuwa kama yanavyotarajiwa.
Danny Welbeck naye ana maumivu
Moyes jana alifungwa mechi ya pili tangu
aanze kazi United katika mechi ambazo tayari wamecheza kwenye ziara yao
na sasa wanaelekea Osaka leo ambako watacheza mechi nyingine Ijumaa.Klabu hiyo inaendelea kuisaka saini ya Cesc Fabregas kutoka Barcelona, lakini wanakabiliwa na ugumu.
Wapinzani wao kama Manchester City
tayari wametumia kiasi kikubwa cha fedha kusajili majira haya ya joto,
lakini United wanasema hawana wasiwasi.
David Moyes amekuwa na mwanzo mgumu Manchester United.