KOCHA Mkuu wa Yanga, Ernie Brandts (Pichani), anatarajiwa kurejea nchini kesho, kabla ya kukiongoza kikosi chake kuivaa Mtibwa Sugar ya Morogoro katika mechi ya kirafiki kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam, keshokutwa.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Ofisa Habari wa Yanga, Baraka Kizuguto, alisema kuwa Mholanzi Brandts ameishamaliza kozi ya siku ya Shirikisho la Soka Ulaya (UEFA) na kwamba kwa sasa yu tayari kurejea kukiandaa kikosi kuelekea ufunguzi wa msimu wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
“Kikosi cha Yanga, Jumapili kinatarajia kushuka ndani ya Uwanja wa Taifa kucheza mchezo wa kirafiki dhidi ya Mtibwa Sugar, mechi ambayo itakuwa ya kwanza kwa Brandts anayerejea nchini kesho kutoka mafunzoni Ujerumani,” alisema Kizuguto.
Brandts alikuwa nchini Ujerumani kwa ajili ya masomo mafupi ya kuongeza muda wa leseni yake ya ukocha ya UEFA, yaliyofanyika kwa siku tatu kuanzia Julai 29 hadi 31, yakihusisha makocha mbalimbali wenye leseni zinazotambuliwa na shirikisho hilo.
Kizuguto alisema kwamba watautumia mchezo huo kuwatambulisha wachezaji wote wapya waliosajiliwa kwa ajili ya msimu mpya wa Ligi Kuu ya Vodacom na klabu bingwa barani Afrika.
Nyota wapya waliotua Jangwani ni pamoja na Deogratius Munishi 'Dida,' Rajab Zahir, Hamis Thabit, Shaban Kondo, Mrisho Ngassa, Hussein Javu na Reliants Lusajo.
Wakati huo huo, Mweka Hazina wa Chama cha Soka Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA), kinachoratibu mchezo huo, Ally Hassan, alisema kuwa taratibu zote zimekamilika.
Hassan alitaja viingilio kuwa ni sh 15,000 kwa VIP A, sh 10,000 VIP B na C, huku viti vya rangi ya bluu, kijani na machungwa ni sh 5,000.