Hatimaye msanii wa muziki wa kizazi kipya nchini, Chid Benzi (Pichani), amekiri kutumia madawa hayo kwa muda mrefu, na kuanza kupatiwa matibabu nchini Kenya.
Akihojiwa katika kipindi cha XXL kinachorushwa na Clouds FM, Benzi alisema ameamua kuanza kutibiwa baada ya kuona hali yake ya kiafya inaanza kuwa tete, na kukiri kutumia madawa hayo na baada ya kuona hayana faida kwake ameona kuna umuhimu wa kuachana nayo.
Kufunguka kwa msanii huyo kumetokea baada ya kuachia kazi yake mpya inayofahamika kwa jina la ‘Nakaza Roho’, ambayo inaelezea jinsi dawa za kulevya zinavyoharibu maisha ya mtu.
Benzi alisema alikuwa ana kazi nyingi katika hazina yake, lakini kulingana na wakati uliopo ameamua kuachia kazi hizo ili wapenzi wa kazi zake wapate somo kuhusu utumiaji wa dawa hizo.
Msanii huyo ni miongoni mwa wasanii waliotamba katika tasnia hiyo kupitia ngoma zake kama ‘Dar Stand Up’, ‘Speed 120’ na nyinginezo ambazo zilimtambulisha na kufanya vizuri katika tasnia ya muziki huo.