come

come
Tuletee habari za kijamii, michezo na burudani, email kabumbu1935@gmail.com

MAKALA: SHAABAN KONDO, STRAIKA MPYA YANGA MWENYE KIU YA KUWATUNGUA MAKIPA

WENGI wanafikiri Yanga iliwafanyia kitu mbaya Simba kuhusu straika huyu mpya wa Yanga aliyekuwa akicheza soka la kulipwa nchini Msumbiji, Lakini ukweli ulivyo sivyo.


Ni zao la Yanga, aliletwa na Yanga huo ndio ukweli wenyewe, Simba walilalamika kuhusu kuporwa kwa straika huyu aliyekuwa akifanya majaribio kwenye uwanja wa Kinesi pale Ubungo.

Ila ilikuwa mipango ya Yanga kujua uwezo wake kwani kikosi cha Yanga kilikuwa bado akijaingia kambini, Simba walianza kambi yao mapea na kutoa nafasi kwa wachezaji mbalimbali kufanya majaribio.

Ndipo Mwanayanga mmoja alipoamua kwa makusudi kumpeleka kwenye mazoezi ya Simba ili kupima uwezo wake, Hatimaye akawaridhisha Yanga kupitia mgongo wa Simba na kupewa mkataba wa miaka miwili kuitumikia Yanga.

Tayari ameanza kuonyesha makali yake katika mechi kadhaa alizopata kucheza, Kiu ya mashabiki wengi wa Yanga ni kuona anaondoa ukame wa mabao uliokuwepo muda mrefu sasa Yanga.

Kondo anaweza kuisaidia Yanga katika upachikaji magoli akisaidiana na washambuliaji wengine sita waliopo Yanga, Didier Kavumbagu, Jerry Tegete, Hamisi Thabit, Said Bahanuzi na Hamis Kiiza kuweza kuing'arisha Yanga.

Ana deni kubwa kulilipa msimu huu unaotarajia kuanza Agosti 24, Pia atakuwa tegemeo katika kikosi cha Yanga kitakachocheza na Azam katika mchezo wa kuwania Ngao ya Hisani kesho uwanja wa Taifa.

Ukimuangalia kwa umbo ni mrefu na mwili uliojazia ambao kocha yoyote akimuona atakubali kuwa anafaa kuchezea nafasi hiyo ya ushambuliaji, Licha ya kucheza taratibu lakini ana uwezo mkubwa wa kumiliki mpira na nguvu jambo ambalo linaweza kuisaidia timu yake kupata mabao ya uhakika kwenye msimu ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Anaitwa Shaaban Kondo (Pichani), kijana mwenye miaka 24 mzaliwa wa Mahenge mkoani Morogoro ambaye amejiunga na Yanga hivi karibuni, Mchezaji huyo amecheza michezo ya kirafiki sita na klabu ya Yanga na kufanikiwa kupachika wavuni mabao mawili ingawa katika mchezo dhidi ya URA  ya Uganda uliofanyika jijini Dar es Salaam mwezi uliopita hakuwa kwenye fomu yake.

“Kweli nilianza mchezo ule taratibu na ilitokana na kutowasoma wapinzani wetu lakini baadaye mbona nilibadilika na kucheza vizuri kwa sababu nilishawajua wapinzani wetu wakoje.

“Lakini pia macho ya mashabiki nayo yalikuwa tatizo kwangu, unajua  kucheza timu kubwa kama Yanga mbele ya mashabiki wengi vile sijazoea hivyo lazima niwe na hofu na ndio maana nilionekana kucheza kwa wasiwasi, lakini  naamini kadri muda unavyoenda nitawazoea na nitacheza kawaida bila presha,” anasema Kondo.

Hata hivyo  mshambuliaji huyo ametoa mpya baada ya kushindwa kuzitaja timu alizokuwa akichezea Msumbiji kwa madai hazijui bali alipelekwa na ndugu yake anayeishi huko.

“ Nilienda Msumbiji mwaka juzi kwa ndugu yangu mmoja na akawa ananitafutia timu nikaenda kufanya majaribio ingawa timu zote nilizoenda walinikataa kutokanana kutoridhika na kiwango changu, wao waliona nipo chini hawawezi kunisajili hivyo ndio nikaamua kurudi Tanzania,” anasema Kondo. 

Habari za uhakika kutoka kwa rafiki yake wa karibu zinasema mchezaji huyo hakuwahi kucheza Msumbiji bali alikuwa nchini na amecheza timu mbalimbali za madaraja ya chini mkoani Morogoro ambazo ni Dimon, Burkina na Bodaboda.

KWANINI ALIITOSA SIMBA!

“Mimi nilipelekwa Simba kufanya majaribio na mtu mmoja wa Yanga kisiri ili anione  uwezo wangu kwani wakati huo Yanga walikuwa hawajaanza mazoezi na baadaye Yanga walipoanza mazoezi ndio nikaenda kufanya nao mazoezi na ndipo wakaridhika na  uwezo wangu na ndio maana nipo mpaka sasa,” anasema Kondo.

Kondo anasema kuwa amejiunga na timu hiyo ili kuhakikisha anatokomeza suala la ukame wa mabao na hivyo mashabiki wavute subira na kusubiri vitu vyake.

“Hapa mimi nimekuja kufanya kazi tu na si kingine kikubwa ni ushirikiano kutoka kwa wachezaji wenzangu ili kuweza kuisaidia timu kupata magoli na kuipa ubingwa', alisema na kuongeza.

'ushindani wa namba ni mkubwa sana hasa katika nafasi ninayocheza lakini lakini sihofii kwani wote ni binadamu kama mimi, nitapambana kuhakikisha nacheza mara kwa mara na nitazingatia  mazoezi, nidhamu ili kuweza kufikia malengo yangu na malengo ya timu pia,” anasema Kondo.

Anaongeza “Yanga ipo vizuri sana na hii inatokana na usajili mzuri uliofanywa na viongozi, pia uongozi ni mzuri na jambo hili linatupa deni sisi kama wachezaji  kujituma zaidi ili tusiwaangushe viongozi na pia mashabiki wetu.

Pia nafurahi hata kocha wetu anavyofundisha, ni kocha mzuri sana  anakuelekeza pale unapokosea na wakati mwingine anakukemea lakini haipaswi kukasirika kwani  ni sehemu ya mchezo na anakufundisha ili uweze kuwa mchezaji mzuri hapo baadaye,” anasema.

Kondo anasema kuwa bado Tanzania ipo chini kisoka ukifananisha na nchi nyingine na hiyo inatokana na kuwa nyuma hata katika masuala ya viwanja vya kufanyia mazoezi na kuchezea mechi na pia hata utendaji mbovu kwa viongozi wengi wanaoendesha soka la nchi hii.

AELEZEA TIMU YA TAIFA

'Mchezaji yeyote yule duniani ana ndoto za kucheza timu ya taifa kisha mipango mingie iendelee, hata mimi nina ndoto za kucheza Stars, nataka kulitetea taifa langu na kuipa heshima katika soka la kimataifa', anasema na kuongeza.

Anadai timu ya taifa ina mapungufu mengi sehemu ya ushambuliaji kwani Tanzania imejaaliwa washambuiaji wengi lakini anashangaa akikosekana Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu timu inapotea, Ipo haja sasa kumtegemea yeye na ili kudhihirisha hilo Watanzania wamshuhudie kupitia ligi kuu ya Vodacom inayotarajia kuanza hivi punde, huyo ndiye Shaaban Kondo