MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Tanzania, Thomas Emmanuel Ulimwengu amesema kwamba ndoto za kuhamia Ulaya zinakaribia kutimia, kwani ana ofa nyingi kutoka nchi mbalimbali, zikiwemo Hispania, Ufaransa, Ubelgiji na Italia.
Akizungumza leo mjini hapa, Ulimwengu aliye kwenye kikosi cha Bara, Kilimanjaro Stars kinachoshirki Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Challenge amesema kwamba ana matumaini makubwa ya kuhamia Ulaya.
“Nina ofa nyingi na zinafanyiwa kazi kwa sasa, nadhani muda si mrefu nitaondoka Afrika, tuombe Mungu,”alisema mshambuliaji huyo wa Tout Puissant Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
Ulimwengu anacheza klabu moja na Mtanzania, mwenzake Mbwana Ally Samatta, TP Mazembe na wote kwa sasa ndiyo wachezaji wakubwa zaidi na tegemeo wa Tanzania.
Wawili hao waliwasili juzi mjini hapa wakitokea DRC, ambako waliichezea klabu yao Fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika na kufungwa jumla ya mabao 3-2 na Sfaxien ya Tunisia. Walifungwa 2-0 ugenini na wakashinda 2-1 nyumbani.
Jana waliichezea Stars mechi ya kwanza ya Challenge dhidi ya Burundi na wakaisaidia kushinda 1-0, bao la Mbwana Samatta pasi ya Mrisho Ngassa. Walikosa bahati tu ya kufunga mabao zaidi, lakini walipata nafasi za kutosha jana Uwanja wa Afraha, Nakuru.
Kwa kuwa Stars imefanikiwa kuingia Robo Fainali, Samatta na Ulimwengu wanatarajiwa kufanya vitu zaidi katika mashindano haya.