Mchezaji maarufu wa tennis wa
Uingereza, Andy Murray amefuzu kucheza hatua ya robo fainali ya michuano
ya wazi ya Mexico baada ya kumtoa Joao Sousa wa Ureno kwa seti 6-3 6-4
katika viwanja vya tenis huko Acapulco.
David Ferrer naye alimcharaza Mhispania mwenzake Feliciano Lopez kwa seti 7-6 (7-1) 6-2.
Grigor Dimitrov wa nne kwa ubora alimng'oa Marcos Baghdatis katika hatua ya robo fainali kwa seti 6-1 6-4 na atapambana na Ernests Gulbis, wa saba katika ubora wa viwango vya tennis ambaye alimfunga David Goffin kwa seti 6-1 3-6 7-6 (7-5).
Murray, ambaye ambaye alikuwa katika kundi moja na Dimotrov na Gulbis, alianza taratibu alipovaana na Sousa - kama alivyofanya katika mzunguko wa kwanza walipokutana na Pablo Andujar.
Bingwa huyo wa Wimbledon aliweza kumtisha Sousa kutokana na upigaji wa mipira na kumlazimisha mchezaji huyo anayeshikilia nafasi ya 44 kwa ubora kuzidi kufanya makosa kutokana na shinikizo alilokuwa akipata kutoka kwa Murray.
Murray sasa atakabiliana na Simon, anayeshika nafasi ya 23, Ijumaa. Mwingereza huyo anajivunia ushindi wa 11-1 dhidi ya Simon katika michezo waliyopambana awali.