SHIRIKISHO la Soka la Kimataifa (SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF) limesema halikuwa na sababu ya kulirudisha suala la mshambuliaji Emmanuel Okwi kwa Kamati ya Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji, kwa sababu taratibu zote za usajili wake zilikwishakamilka na kilichotakiwa ni ufafanuzi wa suala lake kutoka Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA).
Kumekuwa na malalamiko kwamba, kitendo cha Sekretarieti ya TFF kuiandikia Yanga SC barua ya kuwaruhusu kumtumia Okwi bila kwanza kurejesha majibu ya FIFA kwa Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ni kuidharau Kamati hiyo.
Hata hivyo, akizungumza muda huu, Ofisa Habari wa TFF, Boniface Wambura Mgoyo amesema kwamba hakukuwa na sababu ya kulirejesha suala hilo Kamati ya Sheria, kwa sababu kilichotakiwa ni ufafanuzi tu.
“Lile suala huku kwetu lilikuwa limekwishamalizika, taratibu zote za usajili zilikuwa zimekwishakamilika, ila sasa ile Kamati ilitaka ufafanuzi, ambao ulipotolewa na FIFA hatukuona tena sababu ya kurudi nyuma,”alisema Wambura.
FIFA iliiagiza TFF kutazama kanuni zinasemaje juu ya suala la Okwi na baada ya hapo ichukue hatua ya kumuidhinisha au lam, kwa sababu yenyewe haihusiki na masuala ya usajili. Na TFF baada ya kupitia kanuni na kujiridhisha Okwi anaweza kuichezea Yanga, hivyo wakaiandikia klabu hiyo barua ya kumruhusu kucheza.
Januari 22 mwaka huu ikiwa ni siku mbili tu kabla ya kuanza kwa mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya TFF ilisimamisha usajili wa Mganda huyo Yanga ili kwanza upatikane ufafanuzi kutoka FIFA juu ya uhalali wake kucheza timu hiyo ya Jangwani akiwa anatambulika kama mchezaji wa Etoile du Sahel ya Tunisia.
Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya TFF iliyokutana Januari 22, mwaka huu kupitia masuala mbalimbali, ilisema imesimamisha usajili huo baada ya kubaini kuwa Okwi aliruhusiwa kuichezea SC Villa ya Uganda kwa kibali maalumu kutoka FIFA.
Okwi ambaye aliingia kwenye mgogoro na klabu yake ya Etoile du Sahel ya Tunisia aliruhusiwa na FIFA kuchezea SC Villa kwa kibali maalumu (provisional permit) cha miezi sita ili kulinda kiwango chake wakati suala lake dhidi ya Etoile du Sahel likishughulikiwa na shirikisho hilo la kimataifa.
Kulikuwa kuna kesi tatu FIFA kuhusiana na suala la mchezaji huyo, Okwi ameishitaki klabu hiyo FIFA kwa kutomlipa mshahara, Etoile du Sahel imemshitaki mchezaji huyo kwa utoro. Nayo Simba imeishitaki Etoile du Sahel kwa kushindwa kuilipa ada ya mauzo ya mchezaji huyo ambayo ni dola za Marekani 300,000.
Hivyo, TFF iliiandikia FIFA kutaka kujua iwapo mchezaji huyo anaweza kucheza Ligi nchini Tanzania wakati Etoile du Sahel ikiwa imefungua kesi katika shirikisho hilo la kimataifa ikidai Okwi bado ni mchezaji wake na majibu yamewasili TFF Mganda huyo akihalalishwa kuendelea na kazi Yanga.
Lakini bado kuna manung’uniko kwa nini TFF isirejeshe majibu Kamati ya Sheria ili nayo ijiridhishe kutokana na mwongozo wa FIFA itoe baraka zake, ili ikitokea baadaye wakapelekewa Rufaa juu ya mchezaji huyo iwe rahisi kwao kuamua.
Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji inaongozwa na Mwenyekiti Richard Sinaitwa, makamu wake, Moses Karuwa na Wajumbe Zacharia Hans Poppe, Hussein Mwamba, Philemon Ntahilaja, Abdul Sauko na Imani Madega.