Mchezaji mmoja wa Kimataifa wa Morocco,
ambaye alikuwa amepigwa marufuku na shirikisho la mchezo wa soka
duniani, FIFA, amepatikana na hatia ya kutumia madawa ya kusisimua
misuli.
Mchezaji huyo ambaye jina lake halijatolewa, alikuwa amepigwa marufuku ya kutocheza kwa siku thelathini na hatua zaidi za kinidhamu imeanzishwa dhidi yake.
FIFA imsema, marufuku hiyo inahusiana na kosa la kutumia dawa hizo zilizoharamishwa baada ya mechi ya kufuzu kwa kombe la dunia tarehe nane mwezi Juni mwaka huu.
Baada ya kupokea matokea ya uchunguzi wa awali, mchezaji huyo aliiomba shirikisho hilo kurudia tena na matokeo yake yamekuwa sawa.
Uamuzi huo uliochukuliwa na mwenyekiti wa kamati ya nidhamu ya FIFA tayari umewasilishwa kwa shirikisho la mchezo wa soka nchini Morocco.
Mchezaji huyo sasa ana hadi tarehe nne mwezi ujao kuijulisha FIFA ikiwa anataka kesi hiyo kusikilizwa upya.
Hata hivyo shirikisho la soka nchini Morocco linatarajiwa kuwasilisha taarifa yake na ushahidi kwa FIFA kabla ya tarehe kumi na moja mwezi ujao.