Alikuwa akicheza upande wa fulu beki wa kulia lakini baadaye alihamia kiungo cha kati, Jamaa anajua kweli soka kutokana na kasi yake uwanjani na jinsi alivyokuwa anapanga mashambulizi.
Niliumia sana kuona Yanga wakishindwa kumtumia (Telela akiwa pichani kushoto) , Katika michuano hiyo ya kombe la Mapinduzi Yanga ilipeleka kikosi cha pili badala ya kile cha kwanza ambacho nusu ya wachezaji wake walikuwa na timu ya taifa jijini Cairo.
Wakati huo timu ya taifa, Taifa Stars ilikuwa chini ya Mbrazil Marcio Maximo, Nakumbuka Stars ilipata mwaliko maalum katika michuano mipya ya kombe la mafuta iliyoshirikisha nchi zinazotumia maji ya mto Nile.
Taifa Stars iliyokuwa chini ya Maximo ilihusisha wachezaji 10 toka Yanga, Hivyo kombe la Mapinduzi Yanga iliwakilishwa na kikosi chake cha pili na wale wanaokalia benchi.
Hapo ndipo alipochomoza Salum Telela ingawa hakuwa umaarufu mkubwa, Yanga ilifanikiwa kufika fainali ambapo ilijikuta inakutana na Simba iliyokuwa na nyota wake hatari kama Emmanuel Okwi, Patrick Mafisango (Marehemu) na wengineo.
Nakumbuka kabisa Juma Kaseja 'Tanzania One' aliwaongoza Wanasimba katika mchezo huo, Kikosi cha Yanga kilichokuwa na damu changa kilishindwa mbele ya Simba baada ya kulala mabao 2-0 na kuwapa jeuri Simba.
Lakini katika mchezo huo wa fainali, Telela alionyesha kwamba Yanga ina hazina ya baadaye, Alicheza soka la kuvutia na kuwadhibiti wachezaji wa Simba ambao walikuwa wametimia.
Nilipatwa na hofu pale niliposikia usajili wa Yanga ukitangazwa pasipo kuwepo jina la Telela, Moro United ndiyo iliyofanikiwa kumnasa mchezaji huyo ambaye mimi niliona kama mhimili mkubwa wa Yanga katika siku za usoni.
Salum Telela alicheza Moro United kwa mkopo, aliweza kulinda hadhi ya kipaji chake na kufanikiwa kuisaidia timu hiyo kubakia ligi kuu ya Tanzania bara, Moro United iliyokuwa inanolewa na Hassan Banyai iliweza kucheza soka la ushindani na kutokukubali kufungwa na vigogo vya soka nchini Simba na Yanga katika msimu mzima wa ligi.
Ni ngumu timu kama Moro United kushindwa kufungwa hata mechi moja na Simba au Yanga, Lakini kazi nzuri iliyokuwa ikionyeshwa na Telela akishirikiana na wenzake waliifanya Moro United kuwa timu imara.
YANGA WAAMUA KUMREJESHA KIKOSINI
Baada ya kuonyesha kuwa yeye habahatishi, Salum Telela alirejeshwa tena kwenye kikosi cha Yanga, Lakini alipotua tena Yanga alishindwa kabisa kuitumikia timu hiyo na kujikuta akiishia benchi.
Telela hakusikika kabisa ndani ya Yanga na ikafikia hatua alionekana mzigo, Mipango ya kumtema ilikuwepo isipokuwa katika mazoezi anashangaza wengi.
Kusema kweli Telela amekuwa akionyesha kiwango kikubwa mazoezini na kumfanya kocha wa timu hiyo Mholanzi Ernie Brandts na msaidizi wake kukuna kichwa juu ya maamuzi ya kumtema.
Bado aliendelea kuwashawishi Wanayanga na kutaka kuendelea naye, Tatizo lililopo sasa watampanga nafasi ya nani! Kikosi cha Yanga kimeenea kila idara hivyo Telela kuanza katika kikosi cha kwanza ikawa shida nyingine iliyopo.
APATA MAJERAHA AKIWA BENCHI
Wakati kocha Ernie Brandts akiendelea kutafakari, Salum Telela alipata maumivu ya kifundo cha mguu wake, Hivyo alilazimika kukaa benchi kuuguza majeraha yake, Mungu si Athuman, Telela alipona maumivu ya mguu na kurejea tena mazoezini.
Akiwa fiti kuitumikia Yanga msimu huu aliweza kumshawishi kocha wa timu hiyo na kumweka kwenye mipango yake, Brandts aliamini uwezo wa Telela wa kucheza nafasi mbalimbali uwanjani ungeweza kuleta faida kubwa ndani ya Yanga.
Yanga ni timu iliyojaaliwa na viungo wengi mahiri ambao wamekuwa wakionyesha uhai katika mechi kadhaa, Frank Domayo ambaye pia ni tegemeo la timu ya taifa aliumia na kushindwa kuitumikia Yanga.
Hivyo Brandts akaona ni nafasi pekee kumuanzisha Telela, Yanga iliingia vitani kukabiliana na Azam FC katika mchezo wa Ngao ya Jamii wiki mbili zilizopita.
Katika mchezo huo Yanga ilifanikiwa kutwaa Ngao hiyo na kuanza vema msimu mpya wa ligi, Ushindi wa bao 1-0 ulitosha kupeleka shangwe na vigeregere mitaa ya Jangwani na Twiga.
Salum Telela ndiye muuaji wa goli hilo, Lakini soka alilolionyesha siku hiyo lilimuacha kinywa wazi kila shabiki wa soka aliyekwenda kuangalia pambano hilo.
Hapo ndipo Telela alipopata umaarufu na uhakika wa kuanza katika kikosi cha Yanga, Telela anatoboa siri ya goli lake la ushindi kwenye mechi ngumu na kubwa hapa nchini ambapo anadai kuwa ni salamu nyingine kwa mahasimu wao wakubwa Simba ifikapo Oktoba 20