KAMA ni wimbo, sasa umefika kwenye kiitikio. Naam, Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara sasa inaelekea kwenye taswira ya bingwa wa msimu huu, wakati timu mbili zilizo mstari wa mbele kwenye mbio za taji, Yanga SC na Azam zitakapomenyana kesho Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Azam FC ipo kileleni kwa pointi zake 43 baada ya mechi 19, wakati Yanga SC ipo nafasi ya pili kwa pointi zake 39 baada ya mechi 18 na mchezo wa kesho unaweza kutoa picha mpya ya mbio za ubingwa.
Azam na Yanga SC zinaelekea kuwa na upinzani mkali kwa sasa na mechi baina ya timu hizo mara kadhaa zimekuwa zikiingiliwa na vurugu kuanzia uwanjani.
Machi 10, mwaka 2012 wakati Yanga SC ikilala 3-1 mbele ya Azam Uwanja wa Taifa, wachezaji wa timu hiyo walimpiga refa Israel Mujuni Nkongo na mashabiki wao wakafanya fujo kubwa na kuvunja viti, hali ambayo ilifanya Polisi wa kutuliza Ghasia walipue mabomu ya machozi.
Kwa ujumla kesho timu hizo zitakutana kwa mara ya 12 katika Ligi Kuu tangu Azam FC ipande Ligi Kuu msimu wa 2008/2009 na Yanga SC ndiyo iliyoshinda mechi nyingi dhidi ya wapinzani wao hao.
Katika mechi 11 za ligi zilizopita, Yanga imeshinda tano, sare mbili na kufungwa nne, ikifunga jumla ya mabao 16 na kufungwa 14, hivyo kuvuna jumla ya pointi 17 dhidi ya 14 za Azam.
Maana yake, Azam kesho watataka kushinda ili kuwafikia wapinzani wao hao kwa idadi ya mechi za kushinda, kila timu iwe imeshinda mechi tano.
Mchezo wa kesho unatarajiwa kuwa mkali na wa kusisimua kutokana na ukweli kwamba timu zote ziko vizuri kwa sasa, Azam inayofundishwa na Mcameroon Joseph Marius Omog na Yanga ya Mholanzi, Hans van der Pluijm.
Yanga SC itamkosa kipa wake namba moja kwa sasa, Deo Munishi ‘Dida’, lakini mkongwe Juma Kaseja aliyedaka vizuri katika mchezo uliopita dhidi ya Mtibwa Sugar Morogoro anaweza kulinda vyema lango la wana Jangwani hao.
Kwa upande wa Azam, hapana shaka Mwadini Ali ataendelea kulinda lango la timu hiyo ya Alhaj Sheikh Said Salim Awadh Bakhresa na familia yake.
Mbuyu Twite anaweza kuanza katika beki ya kulia Yanga, kushoto Oscar Joshua na katikati safu ya ulinzi itakamilishwa na Kevin Yondan na Nadir Haroub ‘Cannavaro’.
Kwa Azam, Erasto Nyoni anaweza kuanza kulia, kushoto kinda aliyepandishwa kutoka timu ya vijana Gadiel Michael wakati Said Mourad na Aggrey Morris watakamilisha safu ya ulinzi pale katikati.
Kiungo wa ulinzi Yanga SC atakuwa Frank Domayo, wakati kwa Azam bila shaka ataendelea Kipre Michael Balou. Haruna Niyonzima anaweza akaichezesha timu upande wa Yanga, wakati kwa upande wa Azam, hilo linaweza kuwa jukumu la Salum Abakukar ‘Sure Boy’.
Viungo wa pembeni na washambuliaji kwa ujumla, upande wa Yanga inawezekana Pluijm akawaanzisha kwa pamoja Mrisho Ngassa na Simon Msuva pembeni mwa Uwanja na katikati Emmanuel Okwi na ama Hamisi Kiiza au Didier Kavumbangu.
Upande wa Azam pembeni wanaweza kutumia mshambuliaji mmoja Kipre Tchetche na kuongeza kiungo mmoja, Himid Mao ili kuimarisha sehemu yao ya katikati ya Uwanja wakati Brian Umony na John Bocco wanaweza kucheza pamoja katikati mbele.
Unaweza kuona hizo ni timu zenye wachezaji wazuri ambao watatarajiwa kucheza kwa uwezo wao wote katika mchezo muhimu wa kesho.
Wakali watatu; Wachezaji tegemo wa Yanga kutoka kushoto Mrisho Ngassa, Simon Msuva na Didier Kavumbangu, ambao kesho wataongoza safu ya ushambuliaji ya timu yao dhidi ya Azam FC
Bado kwa Yanga benchi wanaweza kuwa wachezaji bora kama Ally Mustafa ‘Barhez’, Juma Abdul, David Luhende, Hassan Dilunga, Nizar Khalfan, Said Bahanuzi, Jerry Tegete, Hussein Javu na Athumani Iddi ‘Chuji’.
Azam pia watakuwa na Aishi Manula ‘Moro Best’, Luckson Kakolaki, Malika Ndeule, Ibrahim Mwaipopo, Jabir Aziz, David Mwantika, Khamis Mcha ‘Vialli’, Gaudence Mwaikimba na Ismail Kone.
Mchezo huo ambao utarushwa moja kwa moja na Televisheni ya Azam TV, utaanza Saa 10:00 jioni Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
REKODI YA YANGA SC NA AZAM FC LIGI KUU
P W D L GF GA GD Pts
Yanga SC 11 5 2 4 16 14 +2 17
Azam FC 11 4 2 5 14 16 -2 14
Septemba 22, 2013; Azam FC 3-2 Yanga SC
Februari 23, 2013; Yanga SC 1-0 Azam FC
Novemba 4, 2012; Azam FC 0-2 Yanga SC
Machi 10, 2012; Yanga SC 1-3 Azam FC
Septemba 18, 2011; Azam 1-0 Yanga SC
Machi 30, 2011; Yanga SC 2-1 Azam FC
Oktoba 24, 2010; Azam FC 0-0 Yanga SC
Machi 7, 2010; Yanga SC 2-1 Azam FC
Oktoba 17, 2009; Azam FC 1-1 Yanga SC
Aprili 8, 2009; Yanga SC 2-3 Azam FC
Oktoba 15, 2008; Azam FC 1-3 Yanga SC
princezub@hotmail.com Mahmoud Zubeiry at 07:14 3/18/2014 09:11:00 AM