come

come
Tuletee habari za kijamii, michezo na burudani, email kabumbu1935@gmail.com

NGASA AREJEA YANGA, KUIMALIZA AZAM MAPEMA

MRISHO Ngassa amefanya mazoezi vizuri na kumaliza kuashiria yuko tayari kwa mchezo wa Jumatano dhidi ya Azam FC Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.

Ngassa aliyewasili kwenye kambi ya timu yake, Yanga SC katika hoteli ya Kiromo, Bagamoyo mkoani Pwani alikosekana katika mchezo uliopita wa ligi hiyo dhidi ya Mtibwa Sugar mjini Morogoro kwa sababu ya majeruhi.

Ngassa alitoka uwanjani kipindi cha pili Jumapili ya wiki iliyopita baada ya kuumia Yanga SC ikimenyana na Al Ahly ya Misri mjini Alexandria katika mchezo wa marudiano Raundi ya Kwanza Ligi ya Mabingwa Afrika na kutolewa kwa penalti 4-3 kufuatia sare ya jumla ya 1-1.

Na baada ya kutua Dar es Salaam Jumatano, alikwenda Mwanza mapumzikoni, huku wenzake wakiingia kambini kujiandaa na mechi dhidi ya Mtibwa Sugar mjini Morogoro Jumamosi iliyoisha kwa sare ya bila kufungana.

Ngassa anatarajiwa kucheza dhidi ya timu yake ya zamani, Azam FC kwa mara ya kwanza msimu huu baada ya kukosa mechi mbili, ya Ngao ya Jamii Yanga ikishinda bao 1-0 na wa Ligi Kuu mzunguko wa kwanza, Azam FC wakishinda 3-2.


Yanga iliyomleta Ngassa Dar es Salaam kwa mara ya kwanza kutoka Kagera Sugar ya Bukoba mwaka 2007, ilimuuza mchezaji huyo Azam FC mwaka 2009, ambao nao mwaka 2012 wakamtoa kwa mkopo Simba SC kumalizia Mkataba wake.

Baada ya kumalizana na Simba SC,
msimu huu Ngassa amerudi timu yake iliyomuingiza mjini na Jumatano anatarajiwa kukutana na Azam kwa mara ya kwanza tangu arejee Yanga.

Ngassa alikosa mechi za awali dhidi ya Azam FC msimu huu kwa sababu alikuwa anatumikia adhabu ya kufungiwa mechi sita kwa kosa la kuhamia Yanga SC akiwa ana Mkataba na Simba SC.

Mtoto huyo wa kiungo wa zamani wa Pamba FC ya Mwanza na Simba SC, Khalfan Ngassa ‘Babu’ anatarajiwa kuwa kivutio kikubwa kwenye mchezo wa Jumatano iwapo atacheza.

Kipa anayeonekana kuwa chaguo la kwanza Yanga chini ya kocha Mholanzi, Hans van der Pluijm, Deo Munishi ‘Dida’ aliyedaka mechi zote dhidi ya Al Ahly na kupangua penalti mbili Uwanja wa Border Guard, aliumia mkono siku moja kabla ya mechi na Mtibwa na Juma Kaseja akaziba vyema pengo lake.

Wazi sasa Kaseja ndiye atakayepewa jukumu la kuzuia michomo ya Azam Jumatano. Mchezaji mwingine atakayekosekana kwenye mchezo wa keshokutwa ni majeruhi wa muda mrefu, kiungo Salum Telela aliyefunga bao pekee katika mchezo wa Ngao.