come

come
Tuletee habari za kijamii, michezo na burudani, email kabumbu1935@gmail.com

FERDINAND AKASHIFU MBINU ZA MOYES

Mlinda ngome nyota, Rio Ferdinand, amekashifu mtindo wa meneja wake David Moyes wa kuchelewa kifichua vikosi vya kuanza mechi za Manchester United.

Moyes hukawia hadi dakika za mwisho kutajia viungo wake ni nani ataingia uwanjani kutoka mwanzo ikilinganishwa na aliyekuwa meneja wa klabu hicho, Sir Alex Ferguson ambaye alikuwa anazindua chake mapema.

Meneja huyo wa zamani wa Everton ameshuhudia mabingwa hao wa Ligi ya Premier ya Uingereza wakiaguka alama 12 nyuma ya viongozi Arsenal na maoni ya Ferdinand ni ishara kuwa wachezaji hawafahamika ipasavyo na mbinu za kinara wao mpya.

“Meneja huyu ni tofauti kiasi kwasababu hasomi kikosi chake mapema,” gwiji huyo aliambia tovuti ya BT Sports kupitia kanda ya video.


“Meneja wa awali alikuwa anatufichulia kama unahitajika au la. Kwa sasa hakuna namna ya kujua kikosi kitajumuisha nani.

“Wakati unajua utacheza, unapata msukumo siku ya mechi na hilo ndilo linalohitajika. Hata kama hutacheza, bado kuna huo msukumo.

“Ni jambo gumu sana akilini kwani unawaza kila wakati kama utajumuishwa au la. Mawazo mazito yanakukumba na wakati mwingine, yanazua hisia za kichaa,” beki huyo wa kati alisema.

Ferdinand hajaorodheshwa kwenye mechi mbili za mwisho za United, sare yao ya 2-2 dhidi ya Tottenham Hotspurs na kuzimwa nyumbani 1-0 na Everton.

United wanakaribisha Newcastle United Jumamosi huku Moyes ambaye bado anasisitiza klabu hicho kina uwezo wa kutetea taji lao akiwapa wachezaji wake changamoto ya kudhihirisha makali yao baada ya kushindwa nyumbani Jumatano.

Kwenye mechi zingine za Jumamosi, Crystal Palace watagwaruzana na Cardiff huku Liverpool ambao wamerejesha moto wakiwaalika West Ham.

Southampton wana kibarua kigumu nyumbani dhidi ya Manchester City ambao wamo katika harakati za kuwania taji la Premier. Magwiji Chelsea watakuwa ugenini Stoke huku West Brom wakitoana manyoya na Norwich.

Sunderland ambao wanavuta mkia watawakaribisha Tottenham kufunga orodha ya Jumamosi.

Viongozi Arsenal watafungua milango ya uga wao wa Emirates kupisha Everton Jumapili katika kinyanganyiro kinacho bashiriwa kuwa cha kata na choka ikitiliwa maanani hali nzuri ya timu hizo kwa sasa.