Mechi inayotarajiwa kuteka hisia za wengi ni kati ya mabingwa watetezi, Uganda The Cranes dhidi ya Tanzania Bara, Kilimanjaro Stars itakayoanza saa 8:00 mchana, ingawa kutakuwa na mchezo mwingine kati ya Kenya na Rwanda saa 10:00 jioni.
Stars wanaingia katika sura ya unyonge kumenyana na The Cranes inayofundishwa na kocha hodari Afrika, Mserbia Milutin Sredojevic ‘Micho’ kutokana na kufungwa mfululizo na wapinzani wao hao siku za karibuni.
Timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars inayoundwa na idadi kubwa ya wachezaji wa Bara ilifungwa nyumbani na ugenini na Uganda katika mechi za kuwania tiketi ya kucheza Fainali za CHAN.
Lakini pia, Uganda imeonyesha ni tishio katika Challenge ya mwaka huu baada ya kufuzu Robo Fainali kwa kushinda mechi zake zote za Kundi C, wakati Bara ilipata ushindi mwembamba wa 1-0 mara mbili na sare moja hivyo kushika nafasi ya pili Kundi B.
Kocha Mdenmark, Kim Poulsen amesema kwamba anawaheshimu Uganda ni timu nzuri na anatarajia mchezo utakuwa mgumu, lakini yeye amewaandaa vyema vijana wake kushinda mechi ya leo.
Micho pia amesema Stars ni wazuri hasa baada ya kuwasili kwa washambuliaji wa TP Mazembe ya DRC, Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu ambao amesema wakiungana na Mrisho Ngassa watetengeneza safu kali ya ushambuliaji.
Kwa ujumla makocha wote wanaogopana kuelekea mchezo huo- jambo ambalo linaashiria hiyo ni mechi isiyotabirika hata chembe.
Kama alivyosema Micho, safu ya ushambuliaji ya Stars leo inatarajiwa kuongozwa na Ngassa, Ulimwengu na Samatta wakati viungo wanaweza kuwa Frank Domayo, Salum Abubakar ‘Sure Boy’ na Athumani Iddi ‘Chuji’.
Langoni ataanza Ivo Mapunda, kulia Himid Mao, kushoto Erasto Nyoni na katikati Said Morad na Kelvin Yondan.
Kwa upande wa mabingwa watetezi, Uganda, Emanuel Okwi, Hamisi Kiiza na Dani Sserunkuma wanatarajiwa kuongoza safu ya ushambuliaji, wakati wengine kikosini watakuwa Nico Wadada, Godfrey Kizito, Khalid Aucho, Brian Majwega, Vincent Kayizzi, Godfrey Walusimbi, Savio Kabugo na Benjamin Ochan langoni.
Emmanuel Okwi ndiye tegemeo la mabao la Uganda Challenge
Kenya inapewa nafasi kubwa ya kuitoa Rwanda katika mchezo wa pili. Je, Stars itafuta uteja kwa The Cranes leo?