Arsene Wenger anahofia kuwa mechi mingi mtawalia mwezi wa Desemba zinaweza poza moto wa viongozi wa ligi ya Premier ya Uingereza Arsenal nyumbani na katika safu za kimataifa.
Ushindi wa 2-0 dhidi ya Hull City Jumatano kupitia mabao ya Nicklas Bendtner na Mesut Ozil ulihifadhi mwanya wa pointi nne katika kilele cha ligi hiyo.
Arsenal pia wananusia kufuzu kutoka msururu wa makundi kwenye Ligi ya Mabingwa na watahakikisha tiketi yao ikiwa wataweza kuwamudu Napoli mnamo Desemba 11.
Kivumbi hicho muhimu kitachezwa kati ya mechi ngumu dhidi ya Everton ambao pia wamenoa makali nyumbani kabla ya kusafiri kichinjio cha Etihad ambapo watamenyana na wapinzani wakuu kwenye harakati za kunyakua taji la Premier, Manchester City siku tatu baada ya kucheza Napoli.
Wenger amelaumu ukosefu wa maelewano kati ya vituo vya runinga ambavyo vinapeperusha mechi moja kwa moja kwa kushinikiza vijana wake kujitosa uwanjani kabla hawajapata mapumziko yanayofaa.
“Tuko na ratiba ngumu ndio maana nililazimika kupumzisha wachezaji wengine,” Wenger alisema baada ya mechi dhidi ya Hull.
“Sasa tunacheza dhidi ya Everton Jumapili na kuna muda mfupi sana kabla ya mechi hiyo na (safari ya) Naples.
“Tunacheza Jumatano usiku Naples na Jumamosi asubuhi dhidi ya Manc City kwa hivyo kwetu, hiyo ni ratiba ngumu sana.”
"Si kusema ni haki au la, ni kwamba hakuna mpangilio baina ya vituo vya runinga. Tungecheza Jumamosi dhidi ya Everton na Jumapili au Jumatatu dhidi ya Man City.
“Si jambo la kawaida kucheza Jumamosi asubuhi na mechi inayofuata ni Jumatatu usiku dhidi ya Chelsea siku kumi baadaye, ikitiliwa maanani muda mchache kati ya mechi ya Ligi ya Mabingwa Jumatano na inayofuata Jumamosi asubuhi,” meneja huyo alieleza.
Everton walisaidia juhudi zao na ushindi wao wa 1-0 ugenini Manchester United katika tokeo lililo waacha mabingwa hao wakidorora alama 12 nyuma ya Gunners.
Licha ya hayo, Wenger alisita kutangaza kwamba matumaini ya United kuhifadhi taji lao yametobuka.
“Hapana, bado ni mapema,” alisema. “Tokeo la Everton ni la mshtuko ndio lakini tumeshuhudia awali wakiziba mwanya wa alama 12 dhidi yetu.”