Mkurugenzi wa Mambo Uwanjani Publishers ambao pia wamiliki wa blogu ya Mambo Uwanjani na Staa wa Leo, Prince Salum Hoza (Pichani) amejitokeza kusaidia kampeni ya upatikanaji wa barabara nzuri na salama inayopitika kwa urahisi katika kijiji cha Kudimoze Matuli tarafa ya Mdaula kata ya Chalinze wilayani Bagamoyo mkoani Pwani ambapo pia ndipo yalipo makazi yake.
Akizungumza na mtandao huu kwa njia ya simu akitokea kijijini kwake Kudimoze ambapo yupo kwa mapumziko mafupi, Hoza amesema ameamua kusaidiana na wanakijiji wenzake ili kuweza kuchonga barabara inayoweza kupitika.
Amedai hadi sasa kijiji hicho akina barabara inayoweza kupitika na magari au pikipiki hivyo imekuwa shida kwa wanakijiji wa eneo hilo kutumia vyombo hivyo, amedai anatumia mbinu ya kuwashawishi wanamichezo hasa vijana kujitolea kwa nguvu zao ili kuchonga barabara hiyo kwa kutumia majembe, makoleo na vifaa vingine.
Hoza ameongeza kuwa ukata ndio unaopelekea kutumia njia hiyo kwani bila ya kujitolea barabara haitaweza kupatikana, aidha Hoza ndiye mlezi wa timu ya soka ya vijana wa kijiji hicho ya Kudimoze FC ambao wamekubali wito huo na muda wowote wataanza kazi ya kuchonga barabara.
Wakati huo huo Hoza amewaomba watu mbalimbali wenye uwezo wa kuwasaidia ili angalau wapate uwezo wa kukodi greda kwa ajili ya kusawazisha vizuri na kupatikana kwa barabara safi na salama, wanakijiji wa Kudimoze hasa akina mama, wazee na watoto hupata shida wakati wakienda hospitali au shuleni kutokana na njia zilizopo hazipitiki kirahisi.
Hata madereva wa magari na pikipiki maarufu kama bodaboda wamegoma kufanya safari katika kijiji hicho kutokana na barabara kutopitika kirahisi hivyo wale wanaokubali kwenda hupandisha gharama za safari kwa abiria.