VIUNGO wa ulinzi wa mahasimu wa jadi, wote ni Wazimbabwe- Simba SC kuna Justice Majabvi na Yanga SC kuna Thabani Kamusoko, wote wamesajiliwa msimu huu. Wote wakongwe, lakini Majabvi ana uzoefu wa kucheza nje ya Zimbabwe kabla ya Kamusoko.
Vizuri wachezaji wote wamefanikiwa kuwateka mashabiki wa timu zao- na hata kuwakuna mashabiki wa mahasimu wao. Sasa kila upande umekuwa unauliza, kati ya Majabvi na Kamusoko nani zaidi?
Katika mechi tatu za Ligi Kuu, kila mchezaji tayari ana bao moja, Majabvi akifunga katika ushindi wa 2-0 dhidi ya Mgambo na Kamusoko akifunga katika ushindi wa 4-1 dhidi ya JKT Ruvu.
Kuwa kuwa wamekuwa wakicheza tangu mwanzo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara na wamecheza vizuri, bila shaka na Jumamosi katika mchezo wa mahasimu wa jadi Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam wataanza.
Kocha Muingereza wa Simba SC, Dylan Kerr amekuwa akimtumia kama sentahafu Majabvi na kiungo wa ulinzi pia na nafasi zote amekuwa akicheza vizuri.
Kocha wa Yanga SC, Mholanzi Hans Van der Pluijm amekuwa akimtumia kama kiungo wa ulinzi na kiungo mchezeshaji Kamusoko na nafasi zote amecheza vizuri. Sasa tunasubiri kuona Jumapili wawili hao wataibukia katika nafasi zipi uwanjani.
Justice Majabvi akiudhibiti mpira dhidi ya mchezaji wa JKT Mgambo
JUSTUCE MAJABVI:
Justice Majabvi aliyezaliwa Machi 26, mwaka 1984 alitua Simba SC mwezi uliopita akitokea Vicem Hai Phong F.C. ya Vietnam na amewahi kuwa mchezaji wa timu ya taifa ya Zimbabwe.
Umaarufu wake nchini Zimbabwe ulikuja wakati anachezea vigogo wa nchi hiyo, Dynamos FC na alikuwemo kwenye kikosi cha klabu hiyo kilichofika Nusu Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka 2008, akicheza jumla ya mechi 14 za mashindano hayo na kufunga bao moja dhidi ya timu ya Swaziland mjini Harare.
Majabvi alijiunga na Dynamos FC mwaka 2006 akitokea Lancashire Steel FC na mwaka 2007 akiwa Nahodha wa klabu hiyo, aliiwezesha kutwaa mataji matatu, ubingwa wa Ligi Kuu ya Zimbabwe, Kombe la CBZ na Kombe la Nestle. Alikuwa Nahodha wa kwanza kushinda ubingwa wa ligi tangu mwaka 1997.
Huyo ni mshindi wa tatu mara tatu wa tuzo ya Mchezaji Bora wa Mwaka wa Zimbabwe, 2005 akiwa Lancashire Steel, 2007 akiwa Dynamos FC na 2008 akiwa Dynamos FC.
Msimu wa 2008–2009 Majabvi alijiunga na Lask Linz FC ya Austria kabla ya kuhamia Khatoco Khan Hoa FC mwaka 2011 aliyoichezea hadi mwaka 2013 alipohamia Vicem Hai Phong F.C. zote za Vietnam, kabla ya kuhamia Simba SC mwezi uliopita. Huyo ndiye kiungo mpya wa Simba SC, Majabvi mwenye uzoefu wa kucheza hadi nje ya Afrika.
THABANI KAMUSOKO:
Zimbabwe anafahamika kama Thabani Scara Kamusoko ‘Rasta’ ambaye alijiunga na Yanga SC mwezi uliopita kutoka FC Platinum ya kwao.
Yanga SC ilivutiwa na mchezaji huyo baada ya kukutana na klabu yake katika Kombe la Shirikisho la Afrika mwaka huu na pamoja kuitoa, lakini ilikunwa na soka ya rasta huyo.
Wakati huo, kilio kikubwa ndani ya Yanga SC kilikuwa ni kiungo mkabaji, hivyo Hans van der Pluijm akapendekeza mchezaji huyo asajiliwe. Wazo hilo likapita katika menejimenti ya Yanga SC na Kamusoko akasajiliwa Jangwani.
Kama ilivyo kwa Majabvi, Kamusoko pia amechezea Dynamos tangu mwaka 2010 alipojiunga nayo kutoka Njube Sundowns aliyoanza kuichezea mwaka 2007 kabla ya kuhamia Platinum FC mwaka jana.
Januari 30 mwaka 2015, Kamusoko alishinda tuzo za Mchezaji Bora wa Msimu na wa Mwaka wa FC Platinums akiwa Nahodha Msaidizi wa kikosi cha mafanikio.
Kamusoko aliyezaliwa Machi 2, mwaka 1988 pia amekuwa akiitwa katika kikosi cha timu ya taifa ya Zimbabwe tangu mwaka 2012, ingawa hajabahatika kuwa na namna ya kudumu kikosi cha kwanza.
Tanzania ni nchi ya kwanza nje ya Zimbabwe kwa Kamusoko kucheza soka- lakini kwa ujuzi wake watu wanasema si wa kiwango cha hapa.
NANI ZAIDI KATI YAO?
Wote mafundi na wanaweza kucheza nafasi zaidi ya moja uwanjani. Wakicheza nafasi za kiungo mkabaji, wanatimiza majukumu yao vizuri, lakini staili zao za uchezaji zipo tofauti.
Wote wanatelezea mipira miguuni mwa wapinzani, wote wanaenda hewani kupiga vichwa, lakini Thabani hapendi kukaa na mpira na ni mara chache kumuona anatembea nao, tofauti na Majabvi ni kawaida kwake kutulia na mpira.
Wanapiga pasi nzuri wote, lakini Thabani ana miguu mirefu na miepesi mno kutoa pasi. Katika ukabaji, Majabvi anaonekana yuko vizuri zaidi na ndiyo maana Kerr amekuwa akimtumia kama sentahafu wakati mwingine.
Katika kuchezesha timu, Kamusoko yuko vizuri, na ndiyo maana Pluijm amekuwa akimpanga kiungo wa juu wakati mwingine.
Simba na Yanga wote wamesajili wachezaji wazuri, tunachosubiri kuona Jumapili ni nani nyota yake itang’ara zaidi ya mwenzake katika pambano la watani.
Chanzo Bin Zubeiry