Mshambuliaji hatari wa mabingwa watetezi wa Ligi Kuu ya Soka Tanzania Bara, Donald Ngoma, amesema anatarajia kiwango chake kuwa juu zaidi na kufunga katika mechi yake ya nne mfululizo wakati watakapowakabili watani wao, Simba, kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam Jumamosi hii.
Mzimbabwe huyo juzi aliifungia Yanga goli moja katika ushindi wa 4-1 dhidi ya JKT Ruvu huku Amissi Tambwe akifunga mawili na Thabani Kamusoko naye alianza kufungua ukurasa wa mabao kwa kupachika bao la nne.
Bao hilo la juzi la Ngoma lilimfanya afikishe magoli matatu msimu huu sawa na Tambwe.
Akizungumza na gazeti hili juzi baada ya mechi, Ngoma, alisema kuwa anajua thamani ya mchezaji wa Yanga huongezeka zaidi pale anapofunga dhidi ya Simba na yeye amejipanga kuhakikisha anawapa furaha mashabiki wa timu hiyo.
Ngoma alisema licha ya kufahamu ushindani utakaokuwepo kwenye mechi hiyo, hana wasiwasi na anaamini ataisaidia timu yake iibuke na pointi tatu.
“Nimeanza kuona ugumu wa ligi, lakini ninaona pia napata uzoefu na kujua cha kufanya, Simba ni watani wa Yanga lakini ni timu kama nyingine, ninaamini nitafunga tena Jumamosi,” alisema mshambuliaji huyo wa zamani wa FC Platinum ya Zimbabwe.
Alisema kuwa anaamini kila mchezaji anaongeza ushirikiano ili kusaka ushindi na kutumia vizuri nafasi tutakazotengeneza.
“Endapo itatokea kama ni mimi kufunga au kutoa pasi, lakini kikubwa Yanga ishinde ili twende na kasi tuliyoianza msimu huu mpya wa ligi,” alisema Ngoma.
Mechi ya Jumamosi itakuwa ni ya kwanza kwa Ngoma kukutana na Simba ambayo imekuwa na rekodi nzuri za kuwafunga Yanga hivi karibuni kila wanapokutana.