Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba jana jioni alisimama kwa dakika tatu mbele ya kipaza sauti lakini akashindwa kuwasilisha Rasimu ya Katiba kutokana na vurugu zilizojitokeza bungeni.
Vurugu hizo zilitokea muda mfupi baada ya Mwenyekiti wa Bunge hilo, Samuel Sitta kumwalika kuwasilisha Rasimu ya Katiba kwa muda wa dakika 120.
Jaji Warioba alisimama kwenye mimbari ya Bunge saa 11:02 jioni tayari kuhutubia lakini kabla ya kufanya hivyo, wajumbe kadhaa walisimama na kuomba mwongozo wa mwenyekiti.
Waliosimama ni Profesa Ibrahimu Lipumba, James Mbatia, Freeman Mbowe na Tundu Lissu.
Hata hivyo, Sitta aliwanyima fursa akisema: “Hakuna mwongozo hapa, naomba Mwenyekiti uendelee, waheshimiwa wabunge hakuna mwongozo naomba Mwenyekiti uendelee kwa ajili ya hansard.”
Kauli hiyo ilionekana kuchafua hali ya hewa kwani Jaji Warioba alipowasha kipaza sauti tayari kuanza kuhutubia, baadhi ya wajumbe walianza kupiga kelele, wengine makofi na kugonga meza hivyo kumfanya ashindwe kufanya kazi hiyo ya uwasilishaji.