MSHAMBULIAJI wa Yanga SC, Mrisho Ngassa amesema Simba na Azam hata wamfuate na makontena ya fedha, hatahama Jangwani.
Akizungumza leo, mtoto huyo wa kiungo wa zamani wa Simba SC, Khalfan Ngassa amesema kwamba anataka kucheza Yanga SC hadi mwisho wa soka yake.
Lakini nyota huyo amesema; “Naweza kuondoka Yanga SC iwapo tu nitapata ofa ya nje ya nchi, lakini kwa sasa akili yangu ni kucheza Yanga hadi mwisho wa soka yangu,”amesema.
Mimi Yanga tu;
Ngassa amesema alitaka kuweka rekodi ya kucheza klabu zote kubwa nchini na anashukuru amecheza Azam FC na Simba SC, hivyo sasa hana mpango wa kuhama Yanga SC.
“Ukiwa mchezaji mzuri, kila klabu itataka huduma yako. Naamini hata Mbeya City wangependa kuwa na Mrisho Ngassa kwa wakati huu, lakini wakati mwingine mtu lazima uwe na maamuzi bila kuyumbishwa na fedha,”amesema.
Mashabiki wa Yanga wananipenda sana, wakati wote nawafikiria wao, namna gani nifanye wafurahi, huwa wananihamasisha kucheza kupita uwezo wangu,”ameongeza Ngassa.
