Anamwaga wino hapo, mkurugenzi wa Bin Slum Tyres Co Ltd Nassor Bin Slum kul;ia akisaini mkataba wa mwaka mmoja na Stand United
NASSOR Bin Slum ni mmiliki wa kampuni ya Bin Slum Tyres Company Limited ambao ni watengenezaji wa matairi ya Double Star na betri zisizoisha chaji za magari RB Battery.
Bin Slum ameingia mkataba mnono wa miaka miwili katikia klabu ya Mbeya City yenye makazi yake mkoani Mbeya wa shilingi Mil 360, Inamaana Mbeya City italamba Mil 180 kila mwaka.
Milionea huyo ameamua kuingia mkataba huo na Mbeya City baada ya kuvutiwa nayo na kuridhishwa na kiwango cha timu hiyo ambayo ilikamata nafasi ya tatu katika ligi kuu ya Vodacom Tanzania bara msimu uliopita.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kusaini mkataba huo, Bin Slum alisema ameamua kuingia mkataba na Mbeya City badala ya vilabu vikongwe vya Simba na Yanga kwa kufuata agizo la rais Jakaya Kikwete ambaye aliwataka wafanyabiashara kujitokeza kuzisaidia timu za mikoani ili kuleta ushindani kwa vigogo hao.
Aidha mfanyabiashara huyo aliahidi kuzisaidia timu zilizopanda daraja za Stand United ya Shinyanga na Ndanda Fc ya Mtwara, haikuchukua muda mara baada ya kusaini mkataba na Mbeya City, Bin Slum aliingia mkataba mwingine na timu iliyopanda daraja ya Stand United ya Shinyanga.
Bin Slum aliingia nayo mkataba wa mwaka mmoja wenye thamani ya shilingi Mil 50, hii inakuwa mara ya kwanza kwa timu za mikoani kupata mikataba minono.
Pia inaonyesha jinsi gani Bin Slum alivyojasili kwa kutoa mamilioni yake kwa timu iliyopanda daraja, anaamini timu hiyo itafanya vizuri kwenye ligi kutokana na kuwapa hamasa pia italeta changamoto.
Ligi ya msimu ujao tutashuhudia timu za Mbeya City na Stand United zikivaa jezi zenye tangazo la Double Star na RB Battery mali za Bin Slum Tyres, ni bahati ya mtende imewaangukia Mbeya City na Stand United huku Ndanda ya Mtwara ikitarajia.
Bin Slum akiwa na mwenyekjiti wa Stand United ya Shinyanga mara baada ya kusaini mkataba wa mwaka mmoja, anaonekana akiwa amevaa uzi wa timu hiyo
Pia udhamini huo utaongeza soko la biashara kwa Bin Slum ambapo sasa mikoa ya Mbeya, Shinyanga na baadaye Mtwara watakuwa watumiaji wakubwa wa bidhaa zinazozalishwa na milionea huyo mzaliwa wa mkoa wa Tanga.
Kwanini Bin Slum ameamua kuzidhamini Mbeya City na Stand United badala ya timu za mkoani Tanga alikozaliwa, Bin Slum alikuwa mkurugenzi wa ufundi wa Coastal Union ya Tanga ambayo ilikamata nafasi ya saba katika msimamo wa ligi.
Bin Slum aliiwezesha Coastal Union kufanya ziara nchini Oman kwa ajili ya maandalizi ya mzunguko wa pili wa ligi kuu ya Vodacom Tanzania bara, timu mbili pekee nchini zilizotoka nje ya mipaka ya Tanzania na kwenda kujifua ughaibuni.
Timu hizo ni Yanga iliyokwenda Uturuki na Coastal Union iliyokwenda Oman, Bin Slum aliifanya Union kama timu yake kwa kujitolea fedha zake pasipo kuandikishana popote, alimwaga mamilioni kununua wachezaji wenye viwango vya juu na vilevile kutengeneza kikosi cha pili cha timu hiyo.
Tulishuhudia kikosi cha pili cha Coastal Union kikiibuka mabingwa wa Uhai Cup kwa kuilaza Yanga B mabao 3-0 katika uwanja wa Chamazi Complex, kikosi hicho pia kilitumika katika mechi za mwisho mwisho za ligi kuu bara.
Kilitoa ushindani mkubwa na kuilaza Simba bao 1-0 katika uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, Coastal Union waliamua kukitumia kikosi hicho baada ya nyota wao kugoma, msimu uliopita Coastal Union iliwasajili Haruna Moshi 'Boban', Juma Nyosso waliokuwa Simba SC.
Wengine ni Jerry Santo, Crispin Odullo, Razack Khalfan, Shaaban Kado, Lutimba Yayo na wengineo, lakini kikosi cha Coastal Union hakikufanya vizuri licha ya Bin Slum kuimwagia zaidi ya mil 400 kama alivyosema wakati akitangaza kujitoa.
Bin Slum akiwa na mshambuliaji wa Coastal Union aliyemnunua Lutimba Yayo
Kilichomwondoa Coastal Union ni mgogoro wa kiuongozi, Bin Slum hakuwa na maelewano mazuri na mwenyekiti wa klabu hiyo Ahmed Ally Aurola, inadaiwa mwenyekiti huyo wa Coastal Union alikataa ushauri wa Bin Slum pamoja na kuingiza wanachama wapya.
Mgogoro huo ulifikia sehemu mbaya kufuatia kulipuana kwenye vyombo vya habari, hivyo Bin Slum akatangaza kujuzuru cheo chake cha ukurugenzi wa ufundi na kubakia mwanachama wa kawaida.
Ndipo alipoanza kuonyesha kufuru yake ya fedha kwa kuingia mikataba na timu za Mbeya City na Stand United, wakati Bin Slum akimwaga mamilioni yake kwa timu hizo za Mbeya na Shinyanga, Coastal Union imetangaza bakuli kwa wakazi wote wa mkoa wa Tanga.
Coastal Union iliwaomba wanamuziki wa kizazi kipya waishio Tanga kuandaa tamasha maalum ambapo fedha zitakazopatikana hapo zitapelekwa kwa klabu hiyo, uongozi wa Coastal Union umekumbwa na ukata unaosababisha baadhi ya nyota wake kuikimbia, hahahaha Coastal Union watajuta kumfahamu Bin Slum.
Picha zote kwa hisani ya Bin Zubeiry Blog
Kwa maoni na ushauri piga 0755 522216.