De La Red alitabiriwa kuwa staa mkali katika soka la Hispania na alikuwamo katika kikosi cha Hispania kilichotwaa Euro 2008 akifunga bao moja dhidi ya Ugiriki katika hatua ya makundi.
Lakini ndoto zake za soka zilikwama wakati alipoanguka uwanjani ghafla kutokana na tatizo la moyo katika pambano la Kombe la Mfalme kati ya Real Madrid na Real Union Oktoba 30, 2008.
Wakati akianguka uwanjani mwaka huo, De la Red alikuwa na umri wa miaka 23 tu na alitabiriwa kuwa staa wa muda mrefu wa Santiago Bernabeu.
Alianguka akiwa peke yake katikati ya uwanja. Umati wote uwanjani ilibidi ukae kimya huku wachezaji wenzake wakiwa wameshika vichwa kwa kukata tamaa. Mmoja kati ya wachezaji hao alikuwa kiungo wa Mali, Mamadou Diarra, ambaye wakati huo alikuwa Real Madrid.
Alitolewa nje akiwa hajitambui na kupelekwa katika vyumba vya kubadilishia nguo. Dakika chache baadaye ilitangazwa kuwa Ruben alikuwa ameamka na tangazo lilipotolewa uwanjani mashabiki wa pande zote mbili waliamka.
Baada ya miaka miwili ya matibabu, madaktari walimshauri De La Red kuachana na soka na alistaafu rasmi Novemba 2010 huku Madrid ikiahidi kuendelea kuwa naye.“Napenda kutoa sapoti kwa wachezaji wote ambao maisha yao ya soka yamekuwa mafupi. Shukrani zangu kwa watu wote ambao wamenisapoti. Nimepigania sana tatizo hili, lakini madaktari wamenishauri niache soka. Siku zote niliota kuwa mwanasoka na kuwa na mafanikio katika klabu hii ambayo ni kubwa duniani,” ndivyo anavyosema.
“Nasubiri kwa hamu kufungua ukurasa mpya wa kazi yangu nyingine klabuni hapa na naishukuru klabu. Nitaendelea kufanya kazi katika klabu hii ambayo naiona kama nyumbani.
Nitajaribu kujifunza ukocha na kupata mafanikio.”Akiwa ni mzaliwa wa Madrid eneo la Mostoles, de la Red alianza kuichezea Real Madrid akiwa na umri wa miaka 14 tu. Baada ya misimu minne akiwa na timu ya vijana ya Madrid, kocha wake, Quique Flores, ambaye alikuwa anahamia Getafe alitaka kufuatana naye lakini Madrid ilikataa.
Aliitwa katika timu ya kwanza na kucheza Novemba 10,2004 katika pambano dhidi ya Tenerife ambalo walishinda mabao 2-1. Lilikuwa la michuano ya Kombe la Mfalme.
Ruben De la Red alipoanguka na ukawa mwisho wake wa kucheza soka la ushindani
Mechi yake ya kwanza La Liga ilikuwa dhidi ya Athletic Bilbao ambapo Madrid walishinda 3-1. Katika msimu wa 2006–07 aliitwa rasmi katika timu ya wakubwa na kocha, Fabio Capello akiwa pamoja na chipukizi wenzake mahiri, Miguel Torres na Miguel Angel Nieto, akacheza mechi saba huku Madrid wakitwaa ubingwa wa La Liga.
Alifunga bao lake la kwanza kwa Madrid Novemba 9, 2006 katika pambano dhidi ya Ecija Balompie michuano ya ndani Hispania na Julai 2007 alisaini mkataba mpya ambao ungemweka Santiago Bernabeu mpaka Julai 2007.
Agosti 31, 2007 de la Red alinunuliwa na klabu ya Getafe ambayo nayo ipo jijini Madrid kwa sharti la kuweza kununuliwa tena na Madrid ndani ya miaka miwili ijayo.
Akiwa na Getafe, de la Red alitisha vilivyo na kuwa mchezaji muhimu klabuni huku akiungana na staa mwingine kinda wa Madrid, Esteban Granero aliyepelekwa kwa mkopo.Katika msimu huo, kutokana na majeruhi, Getafe ililazimika kumtumia de la Red katika nafasi ya beki wa kati.
Katika pambano la robo fainali la Kombe la Uefa dhidi ya Bayern Munich, de la Red alikuwa katika kiwango cha juu ingawa katika pambano la marudiano alipewa kadi nyekundu katika dakika ya sita tu.
Katika michuano hiyo, de la Red alifunga mabao matatu katika mechi 11 huku akikumbukwa kwa kufunga bao la kusawazisha katika pambano dhidi ya Tottenham baada ya kupokea pasi murua kutoka kwa Granero.
Mei 2008, Rais wa Real Madrid, Ramon Calderon, alithibitisha kwamba Granero, Javi Garcia na de la Red wangerudi tena katika kikosi cha Santiago Bernabeu kwa msimu wa 2008–09. Ilidaiwa kwamba de la Red alirudishwa kama chambo kwa ajili ya kubadilishana na wachezaji mastaa wa timu nyingine ambao kocha Bernd Schuster angewahitaji.
Alifunga bao lake la kwanza Agosti 24, 2008 katika pambano la pili la fainali za Super Cup dhidi ya Valencia akipiga shuti la mbali. Akafunga la kwanza la Ligi Septemba 21 dhidi ya Racing Santander.Oktoba 30, 2008 ndipo de la Red alipokumbana na janga la kuanguka uwanjani katika pambano dhidi ya Real Union na hivyo kuhitimisha maisha yake ya soka miaka miwili baadaye baada ya madaktari kumshauri hivyo.