Frank Lampard ametangaza kustaafu kucheza soka la kimataifa. Kiungo huyo, aliyejiunga na Manchester City kwa mkopo akitokea New York City, alicheza mechi yake ya mwisho kama nahodha wa England katika sare ya 0-0 dhidi ya Costa Rica katika michuano ya Kombe la Dunia, mwezi Juni.
Kiungo huyo wa zamani wa Chelsea, 36, ameichezea timu yake ya taifa mara 106, tangu Oktoba mwaka 1999, alipocheza mechi yake ya kwanza dhidi ya Ubelgiji.
Lampard amecheza katika michuano mitano mikubwa na kupachika mabao 29. Anakuwa mchezaji wa sita kuwahi kuichezea England mara nyingi zaidi sawa na Sir Bobby Charlton. Lampard, aliyeanza kucheza soka la kulipwa katika klabu ya West Ham, aliondoka Chelsea msimu uliopita baada ya kuichezea klabu hiyo mara 648 na kufunga magoli 211.