come

come
Tuletee habari za kijamii, michezo na burudani, email kabumbu1935@gmail.com

WAZEE YANGA WAISHIKA PABAYA SERIKALI,WAIPA SIKU TANO KUPITISHA UWANJA WAO.

Uongozi wa klabu ya Yanga umeipa siku tano Halmashauri ya Manispaa ya Ilala kutoa idhini ya kujenga uwanja wa kisasa katika eneo la Jangwani jijini Dar es Salaam huku ukitishia kufanya maandamano endapo haitatekelezewa hitaji hilo.

Akizungumza na waandishi wa habari kwenye ofisi za makao makuu ya klabu hiyo zilizopo makutano ya mitaa ya Jangwani na Twiga jijini jana, Katibu wa Baraza la Wazee la Yanga, Ibrahim Akilimali alisema wamebaini klabu yao inawekewa vikwazo na baadhi ya madiwani wa manispaa hiyo katika kufanikisha ujenzi wa uwanja huo walioupa jina la 'Jagwani City'.

“Jana (juzi) kulikuwa na kikao cha Baraza la Madiwani hapa Dar es Salaam na uongozi wa Yanga uliomba uhudhurie kikao hicho kwa sababu moja ya ajenda ilikuwa ombi la klabu yetu kuongezwa eneo na kibali cha ujenzi wa Jangwani City. Cha kushangaza tulikatazwa kuingia kwenye kikao hicho na kukalishwa nje ya ukumbi kwa saa 10,” alisema Akilimali huku akisisitiza kuwa alikuwa amepewa idhini ya kuzungumza hayo na uongozi wa klabu hiyo.

Ilikuwa mara ya kwanza jana Akilimali kuzungumzia masuala ya Yanga tangu azuiwe na uongozi kuzungumza na vyombo vya habari kuhusu mambo ya Yanga katika mkutano mkuu uliopita wa wanachama wa klabu hiyo uliofanyika jijini Dar es Salaam Januari mwaka huu.


“Tumebaini tunawekewa 'kauzibe' katika kufanikisha suala hili zuri kunakofanywa na baadhi ya viongozi waliochaguliwa na wananchi.

Tunakipenda chama chetu cha CCM na Yanga ndiyo mwanzilishi wa chama hicho kwa sababu hata Mwenyekiti wa Kwanza wa TANU (Mwl. Julius Nyerere) ndiye aliyekuwa mwanachama mwenye kadi nambari moja ya Yanga," alisema zaidi Akilimali ambaye alikuwa amefuatana na Mwenyekiti wa Vijana wa Yanga, Bakili Makele na viongozi wengine wa Baraza la Wazee la klabu hiyo.

“Kama wameamua kumwaga mboga, na sisi (Yanga) tutamwaga ugali 2014 na 2015 kwa sababu Yanga imekuwa ikisaidia sana CCM kufanya vizuri katika masuala ya siasa.

Uwanja wetu utakuwa na faida kubwa kwa serikali ambayo itapata mapato. Tunashangaa kuwekewa kauzibe na viongozi wetu.

“Tunawapa siku tano watupe jibu vinginevyo tutaomba kibali Jeshi la Polisi ili wanachama wa Yanga tuandamane. Maandamano yetu tutayaelekeza kwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam ambaye alifika hapa mwaka jana na kuagiza suala letu lishughulikiwe lakini mwaka mzima sasa linapigwa danadana. Maandamano yetu pia tunaweza kuyapeleka kwa Mkuu wa nchi kwa sababu watendaji wake wanakiuka Ilani ya chama tawala na mipango ya serikali katika kuinua michezo nchini.”

Hata hivyo, viongozi wa Yanga walipotafutwa na NIPASHE kuzungumzia vitisho hivyo vya Akilimali na wenzake, hawakuwa tayari kueleza kuhusu ruhusa ya kutolewa kwa tamko hilo.

Katibu Mkuu wa Yanga, Beno Njovu alikataa kuzungumzia suala hilo kwa kusema: "Mtafute Ofisa Habari, atakueleza vizuri."

"Sikuwapo wakati wa mkutano huo, hivyo sijui idhini ya kuzungumza na vyombo vya habari Akilimali amepewa na kiongozi yupi wa Yanga," alisema Baraka Kizuguto, Kaimu Ofisa Habari wa Yanga katika mahojiano na NIPASHE jijini jana jioni.

HALMASHAURI  ILALA WALONGA
Wakati Yanga wakitoa vitisho hivyo, uongozi wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilala umesema maombi ya Yanga yanashughulikiwa na vitengo vyake vinavyohusika na ardhi, ujenzi na mipango miji.

Lucy Semindu, Ofisa Habari wa Manispaa ya Ilala, aliwaambia waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana kuwa, wamepokea maombi ya uongozi wa Yanga kuhusu ujenzi wa uwanja wa kisasa na watatoa tamko baada ya wataalam wa vitengo vya ujenzi, ardhi na mipango miji kukagua eneo husika.