Mahakama nchini Ujerumani
imemhukumu rais wa klabu bingwa Ulaya, Bayern Munich, Uli Hoeness,
kifungo cha miaka mitatu na miezi sita jela kwa kukwepa kulipa kodi.
Licha ya wakili wake kuiomba mahakama kutomwadhibu Bw Hoeness kwa sababu ya kujisalimisha kwake, mahakimu waliafikia kwamba Hoeness hakukiri kikamilifu.
Hapo awali Hoeness alishtakiwa kwa kukwepa kulipa ushuru wa euro milioni 3.5 (£2.9m; $4.9m) lakini baadaye akakiri kuwa hajawahi kulipa milioni nyingine 15.
Hatimaye Alhamisi, korti ilibaini kuwa alikosa kulipa ushuru wa jumla ya euro milioni 27.2.
Upande wa utetezi umesema kwamba utakata rufaa dhidi ya uamuzi huo.
Hata hivyo Hoeness atabakia kuwa huru hadi uamuzi wa mwisho kabisa utakapotolewa.