come

come
Tuletee habari za kijamii, michezo na burudani, email kabumbu1935@gmail.com

AFC LEOPARDS YAMRUDISHA LOGA KENYA.

Wakati klabu ya soka inayoshiriki Ligi Kuu ya Kenya, AFC Leopalds ya Kenya ikitajwa kuanza mazungumzo na Kocha Mkuu wa Simba, Zdravko Logarusic, Mcroatia huyo ameweka wazi kwamba anahitaji kuongezewa mshahara kwenye mkataba wake mpya endapo ataendelea kubaki nchini kuinoa.

Logarusic ambaye alitua nchini mapema Desemba mwaka jana na kusaini mkataba wa miezi sita na Simba unatarajiwa kumalizika Mei 31, mwaka huu, kwa sasa mshahara anaolipwa ni Dola za Marekani 3,000 kwa mwezi.

Akizungumza jana, Logarusic, alisema anaheshimu mkataba wake na Klabu ya Simba ingawa aliweka wazi kuwa anahitaji kuboreshewa maslahi yake.

Logarusic alisema ni mapema kuzungumzia mkataba mpya kwa sababu bado hajamaliza mkataba wa awali na anaamini muda sahihi utakapofika watazungumza na viongozi.


"Mimi ni Kocha wa Simba, siwezi kuzungumzia klabu nyingine kwa sasa," alisema kwa kifupi kocha huyo.

Aliongeza kwamba atafurahia kuendelea kubaki nchini na anaamini timu yake itakuwa bora zaidi kwenye msimu ujao kwa sababu atashiriki maandalizi ya kusajili wachezaji anaowahitaji.

"Mpaka sasa nafurahia kuwa Simba, hakuna tatizo, changamoto ninazokutana nazo kwa hapa Afrika ni za kawaida," Logarusic aliongeza.

Mmoja wa viongozi wajuu wa Simba aliliambia gazeti hili kuwa kocha huyo ana nafasi kubwa ya kupewa mkataba mpya na tayari ameelezwa ataenda kwao kwa likizo fupi ya siku saba kusalimia familia na kutakiwa kuwahi kurudi nchini kuendelea na zoezi la usajili wa wachezaji.

Pia katika kuanza maandalizi ya msimu ujao wa ligi, Mkurugenzi wa Ufundi wa klabu hiyo, Moses Basena, amepewa jukumu la kwenda kwao Uganda kuangalia wachezaji wanaofaa kuongeza kwenye kikosi cha Simba.

Katibu Mkuu wa Simba, Ezekiel Kamwaga, alipoulizwa alisema Kamati ya Utendaji ya klabu hiyo ndiyo itakayotoa maamuzi ya kumpa mkataba mpya au la na bado haijakutana kujadili suala hilo.

Logarusic alianza kwa kishindo kwa kuifunga Yanga mabao 3-1 kwenye mchezo wa Nani Mtani Jembe.