come

come
Tuletee habari za kijamii, michezo na burudani, email kabumbu1935@gmail.com

LOEW AOMBA MASHABIKI WAUNGE MKONO WACHEZAJI

Joachim Loew

Kocha wa Ujerumani Joachim Loew ametoa wito kwa mashabiki kuunga mkono wachezaji wake wakati wa mechi ya kufuzu kwa Euro 2016 Jumapili dhidi ya Scotland mjini Dortmund.

Ametoa wito huo baada ya mashabiki kumzomea straika Mario Gomez wakati wa mechi ya kirafiki dhidi ya Argentina Jumatano. Baadhi ya mashabiki wa Dortmund pia hawajamsamehe kiungo wa kati Mario Goetze kwa kuhama klabu hiyo na kujiunga na Bayern Munich.

"Si haki kuzomea wachezaji wenu. Hilo huwa halisaidii mchezaji na timu pia,” Loew aliambia wanahabari mjini Kamen Jumamosi.

"Dortmund itatuunga mkono,” alisema kuhusu mapokezi yanayotarajiwa Jumapili ya straika wa Fiorentina Gomez na Goetze, aliyefungia Ujerumani bao la ushindi wakati wa ushindi wao wa 1-0 fainali ya Kombe la Dunia dhidi ya Argentina.


Loew alisema anatarajia mashabiki mjini Dortmund Jumapili “washerehekee” timu hiyo kama mabingwa wapya wa dunia.

Ingawa Goetze amezomea na mashabiki wa Dortmund tangu ahamie Bayern, Loew alisema: “Kesho yeye ni mchezaji wa timu ya taifa. Naamini mashabiki Wajerumani watamshabikia Mario Goetze mjini Dortmund."

Goetze huenda aanze kama straika aliyefichwa, huku Gomez – aliyeanza wakati wa kichapo chao cha 4-2 mikononi mwa Argentina mjini Dusseldorf – akitarajiwa kuwa benchi.

Loew alimtetea Gomez, aliyekosa nafasi nyingi nzuri dhidi ya Argentina, kama straika wa hali ya juu, ambaye amerudi kwenye kikosi baada ya kukosa Kombe la Dunia kutokana na jeraha.

Lazima watu wamwelewe Gomez, ambaye amefunga mabao 25 katika mechi 60 akichezea Ujerumani, ikizingatiwa kwamba ni mapema sana msimu huu na amechezea Fiorentina mechi moja pekee ligini, Loew alisema.

"Mario akiwa katika hali nzuri, huwa matata sana, mmoja wa mastraika wakali zaidi duniani,” akasema.
Ujerumani wanakosa wachezaji kadha waliocheza sana Kombe la Dunia, huku nahodha Bastian Schweinsteiger, difenda Mats Hummels na viungo wa kati Mesut Oezil na Sami Khedira wakiwa hawako.
Jerome Boateng wa Bayern Munich amerudi baada ya kuuguza jeraha la goti na atasaidiana na Benedikt Hoewedes wa Schalke safu ya kati ya ulinzi kwenye mechi hiyo ya Kundi D.

Loew alisema anatarajia vita vikali dakika hizo 90 dhidi ya Scotland ambao hawajashindwa katika kipindi cha mwaka mmoja.

"Wachezaji hao wa Scotland watakuwa wakali sana. Hawana lolote la kupoteza dhidi ya mabingwa wa dunia,” Loew alisema.