come

come
Tuletee habari za kijamii, michezo na burudani, email kabumbu1935@gmail.com

MAKALA: MSHAMBULIAJI WA KATI SIO LAZIMA AJUE KUPIGA CHENGA

Na Fikiri Salum

KELELE zimeanza hasa baada ya mshambuliaji mpya wa Yanga Mbrazil Genilison Santos Santana 'Jaja' kushindwa kuwaridhisha mashabiki wa soka wanaokwenda kumtazama uwanjani akiwa na kikosi chake cha Yanga.

Kelele hizo zimeanza kutolewa na mashabiki hasa wanaodaiwa kuwa ni watani wao wa jadi Simba SC ambao kawaida yao kubeza kikosi cha Yanga hata kama kinaonyesha makali.

Mashabiki hao wamekuwa wakimbeza zaidi Jaja kwa kushindwa kuonyesha makeke yake kama ilivyo kwa wenzake wanaocheza safu ya ushambuliaji.


Pia wapo baadhi ya mashabiki wa Yanga ambao nao hawaridhishwi na kiwango cha Mbrazil huyo huku wakipeleka shutuma zao kwa uongozi wa timu pamoja na kocha Marcio Maximo.

Kwa sasa Maximo anabeba mzigo wa lawama kwa kukubali uwepo wa Mbrazil huyo na kubaliki kukatwa kwa mchezaji huyo kipenzi Emmanuelo Okwi ambaye kwa sasa amejiunga na watani zao Simba.

Okwi ametua Simba na kuzua sekeseke katika kwa viongzi wa Yanga kiasi kwamba mwenyekiti wa timu hiyo Yusuf Manji kuzungumza na waandishi wa habari na kukanusha kuwa hawajamkata Okwi na wanataka TFF iingilie kati usajili wake Simba ama sivyo wataenda FIFA au CAS.Yanga ilikuwa tayari ina wachezaji watano wa kigeni ambao ni Wanyarwanda Haruna Niyonzima, Mbuyu Twite, Waganda Emmanuel Okwi na Hamisi Kiiza pamoja na Mbrazil Andrey Coutinho.

Kuongezeka kwa Mbrazil mwingine Jaja kumeifanya Yanga kuwa na idadi ya wachezaji wa kigeni sita hivyo kwa mujibu wa sheria za TFF ambazo zinataka kila klabu kuwa na wachezaji watano wa kigeni kumeifanya Yanga kufikiria kukata jina la mchezaji mmoja.

Wakati akiwasili nchini kwa mara ya kwanza, Jaja anaambiwa ajui hata kupiga chenga

Awali Yanga iliweka mezani jina la Hamisi Kiiza kwa ajili ya kukatwa lakini Kiiza aliwahi kuropoti mazoezini na kumfanya kocha Marcio Maximo kumuona na kuridhishwa na kiwango chake.

Kasheshe lilibaki kwa Okwi ambapo kwa niaba ya kocha Maximo alipendekeza Mganda huyo akatwe katika idadi yake ya wachezaji wa kigeni kwa vile ajaripoti mazoezini tangia alipoanza kufanya nao.

Utoro wa Okwi umemfanya Maximo apendekeze majina ya wachezaji watano huku Okwi akitemwa, wakati Maximo akifanya hivyo uongozi wa Yanga ulikuwa katika mgogoro mkubwa na kiungo huyo wa kimataifa ambapo uongozi ulisema unataka Okwi arudishe gharama zao za usajili kutokana na utoro wake.

Yanga walimsajili Okwi katika usajili wa dirisha dogo kwa mikataba wa miaka miwili na nusu lakini ameitumikia Yanga miezi sita tu na kutoroka kambini akiicha Yanga haijamaliza mechi zake saba za mwisho na kusababisha Yanga kuutema ubingwa wake mbele ya Azam FC.

Uongozi wa Yanga haukuridhia kutemwa Okwi na ulitaka atemwe Jaja kutokana na uwezo wake kuonekana mdogo mazoezini, Jaja ni mzito hivyo anawapa wasiwasi Wanayanga.

Licha ya Yanga kuweka kambi yake viziwani Pemba baadaye Unguja na kucheza mechi tatu na majaribio, uwezo wa Jaja haukuwaridhisha wengi, wengi walitilia mashaka kiwango chake na kumbeza huku wakidai ni garasa kama magarasa wengine waliopata kuichezea Yanga miaka ya nyuma.

Yanga ilianza kucheza mechi zake za kirafiki na Chipukizi ya Pemba na kuibuka na ushindi mwembamba wa bao 1-0, goli hilo liliwekwa kimiani na Jaja kwa njia ya kichwa, ilielekea Unguja na kucheza mechi mbili za kirafiki.

Mechi yake ya kwanza ilicheza na Shangani ambapo ilishinda tena 1-0 likifungwa na Andrey Coutinho kabla haijacheza na mabingwa wa Zanzibar KMKM na kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 yaliyofungwa na Salum Telela na Coutinho.

Katika mechi zote hizo mbili, Jaja alishindwa kung'ara, Jumatano iliyopita Yanga ilicheza mchezo wa kirafiki wa kimataifa na timu ya ligi kuu nchini Kenya Thika United kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam na kuibuka na ushindi wa 1-0.

Goli la Yanga liliwekwa kimiani na Mbrazil Jaja, licha ya kufunga goli hilo wengi walihoji kiwango chake na kudai ni mzito mno na hafai kuitumikia timu hiyo, si mashabiki tu ndio waliombeza safari hii hadi wachezaji wa timu ya Thika United ya Kenya ambapo walisema kiwango cha mshambuliaji huyo ni kidogo na wala hafai kuichezea Yanga.

Moses Odhiambo ambaye aliwahi kuichezea Yanga miaka ya nyuma amesema kiwango cha Mbrazil huyo akimridhishi hata kidogo na anausifu uwezo wa Simon Msuva na Coutinho, wanasema Jaja awezi kutuliza mpira wala kupasua ukuta hivyo hana uwezo wa kuichezea Yanga.

Anajua kufunga huyu: Wanayanga wametakiwa kumuamini tu mshambuliaji wao wa kati kwani kazi yake moja tu kufunga na si kucheza na jukwaa

Wapo pia baadhi ya wadau wanaona kama Yanga imepotea kwa kumtema Okwi na kumbakiza Jaja, lakini wanashindwa kuelewa kuwa Okwi ni kiungo mshambuliaji na Jaja ni mshambuliaji wa kati yaani straika.

Sifa za watu wawili ziko tofauti, Okwi anatakiwa awe anatafuta mipira kwa hali na mali na kumpelekea straika ili aweze kufanya yake, ndio maana Okwi hakuweza kuifungia Yanga mabao mengi kwavile kazi yake si kufunga isipokuwa ni kutafuta mipira na kuanzisha mashambulizi.

Waliombeza Okwi kwanini akufunga magoli alipokuwa Yanga hawajui soka, na wanaombeza Jaja kwanini ajui kupiga chenga pia hawajui soka, kazi ya mshambuliaji wa kati ni moja tu kufunga, na Jaja amefanya hivyo anajua kufunga iwe kwa kichwa sawa, kwa mguu sawa ili mradi ajue kufunga.

Nadhani hapo mmenielewa, haku haja ya kuumiza kichwa ooh Jaja ajui kupiga chenga mara ooh mzito hilo sio tatizo, uwezo wa Jaja ni kufunga tu, tena ni mtaalamu wa vichwa, anatukumbusha enzi za Abeid Mziba 'Tekelo', Ijumaa Karimu, 0755 522216.