Mshambuliaji wa Simba, Raphael Kiongera amegoma kupokea jezi namba 5 kwa madai kuwa hawezi kuivaa badala ya Donald Mosoti na kutaka atafutiwe namba nyingine.
Meneja wa timu hiyo, Nico Nyagawa alisema juzi kuwa Kiongera atakuwa anatumia jezi hiyo lakini mambo yakawa tofauti baada ya mshambuliaji huyo kugoma.
Kiongera aliomba apewe jezi namba 29, lakini pia ilikuwa ngumu kuipata kwani tayari namba hiyo alipewa beki Adam Miraji.
Akizungumza na gazeti hili juzi, Kiongera alisema namba anazopenda kuzitumia ni 5 na 29, lakini zote zinatumiwa na wachezaji wengine, ambapo viongozi wake wamedai kumpa namba 12, lakini namba hiyo ameikataa.
“Mosoti bado yupo kwenye timu, wananipaje namba anayovaa yeye, siwezi kuvaa namba hiyo, awali walinipa namba 29 ambayo pia naipenda, lakini nimekuta wamempa mchezaji mwingine na wananilazimisha kuchukua namba 12 ambayo siipendi,” alisema Kiongera.
Mchezaji huyo alijiunga na kambi hiyo Jumatatu na kuanza rasmi mazoezi yake Jumanne, ambapo kocha Patrick Phiri alisema atampa mazoezi maalumu kwa muda wa wiki moja ili awe sawa na wenzake walioanza maandalizi muda mrefu.
Phiri alisema Kiongera atakuwa anafanya mazoezi ya ufukweni na uwanjani, mazoezi ambayo mshambuliaji huyo amelalamika kuwa ni magumu.
“Nimepewa mazoezi magumu lakini yananijenga kuwa ‘fiti, unajua sijafanya mazoezi na wenzangu, nitahakikisha nafanya kwa bidii ili niwe sawa nao,” alisema.Wakati huo huo, usajili wa beki Shaffih Hassan umekwama na kuifanya Simba kumpoteza beki huyo katika safu yake ya ulinzi.
Hassan alijiunga na Wekundu wa Msimbazii mara baada ya kikosi hicho kutua Zanzibar na kucheza mchezo wa kirafiki dhidi ya KMKM.