Kiungo mpya Andrey Cotinho wa Yanga amesema amebaini kwamba ana deni kubwa la kuwalipa wapenzi wa klabu hiyo baada ya kumpokea kwa shangwe katika mechi yao ya kimataifa ya kirafiki waliyoshinda 1-0 dhidi ya Thika United kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam juzi.
Mashabiki wa Yanga waliokuwa wamefurika kwenye uwanja huo uliokuwa mkubwa kuliko vyote barani Afrika kabla ya kujengwa kwa Uwanja wa Soccer City nchini Afrika Kusini 2010, walimshangilia mwanzo - mwisho raia huyo wa Brazil kutokana na chenga zake zilizojaa kila aina ya fedheha.
Mara tu baada ya mechi hiyo kumalizika, Cotinho aliiambia Staa wa leo kuwa amejisikia mwenye deni kubwa kwa Wanayanga kutokana na mapokezi mazuri waliyoyaonesha kwake.
"Sikutarajia kupokewa kwa furaha namna hii. Ninajiona mwenye deni kubwa kwa watu hawa. Ninaamini wana matumaini makubwa kutoka kwangu na ninapaswa kuwafanyia mazuri," alisema Cotinho.
Aidha, kiungo huyo ambaye juzi alichezeshwa kama winga wa kushoto, alimmwagia sifa kiungo wa kimatifa wa Yanga, Haruna Niyonzima ‘Fabregas’ na kuweka wazi kuwa Mrwanda huyo ana kipaji kikubwa cha soka.
“Tangu nitue hapa nimeona baadhi ya wachezaji wana uwezo mkubwa, kuna mchezaji wetu anavaa jezi namba nane (Niyonzima) ana uwezo mkubwa sana. Baadhi ya mambo nimeanza kuiga kwake,” alisema.
Cotinho na mshambuliaji wa kati Genilson Santana Santos ‘Jaja’ anayetoka pia Brazil, wamesajiliwa na Yanga msimu huu kwa pendekezo la kocha mpya wa timu hiyo Mbrazil Márcio Máximo.
Katika mechi ya juzi Cotinho, aliyeteka vichwa vya magazeti ya michezo nchini tangu atue kuitumikia Yanga, alicheza kwa dakika 70 kabla ya kupumzishwa na nafasi yake kuchukuliwa na kiungo mkongwe Nizar Khalfan.