Dar es Salaam. Baada ya kutwaa ubingwa wa soka Tanzania Bara,
wachezaji wa Yanga kila mmoja anatarajiwa kuvuna Sh3.3 milioni zikiwa ni
zawadi za kutwaa ubingwa huo.
Yanga ilitwaa ubingwa mwaka huu huku ikiuhalalisha
kwa kuwalaza watani wake Simba mabao 2-0 katika mchezo wa funga dimba
uliofanyika kwenye Uwanja wa Taifa, Mei 18.
Chanzo cha habari kutoka ndani ya Yanga kinasema
kuwa fedha zilizopatikana mpaka sasa ni Sh230 milioni baada ya kutwaa
ubingwa huo.
Chanzo hicho kilisema kuwa fedha zilizotengwa kwa
wachezaji ni zile za ubingwa Sh70 milioni kutoka Vodacom, Sh50 milioni
(Supersport), Sh80 milioni (klabu) na wadhamini wa klabu hiyo Kampuni ya
Bia Tanzania (TBL) wanaotoa Sh30 milioni.
“Siwezi kukwambia wachezaji watakaopata wako
wangapi, lakini ninachofahamu wachezaji wote watapata Sh3.3 milioni
wakati benchi la ufundi na watu wengine walioisaidia timu kutwaa ubingwa
watapata zawadi kwa nafasi zao,” kilisema chanzo hicho cha habari.
Chanzo hicho cha habari kinasema kuwa, “wachezaji
wa Yanga watapewa fedha hizo katika sherehe kubwa ya kuwapongeza pamoja
benchi la ufundi na viongozi baada ya kumalizika kwa michuano ya Kombe
la Kagame mapema mwezi ujao.”