Ingawa historia inasema Yanga ilianzishwa mwaka 1935 na Simba mwaka
1936, lakini ukizama ndani utagundua kwamba , huo ndiyo ulikuwa mwanzo
wa utani na upinzani wa jadi baina ya miamba hiyo ya soka nchini.
Kulikuwa kuna timu inaitwa New Youngs ambayo mwaka 1938 ilisambaratika
na baadhi ya wachezaji wake wakaenda kuunda timu iliyokuwa Sunderland,
ambayo hivi sasa inajulikana kama Simba.
Kabla ya kutokea vurugu zilizoisambaratisha New Youngs vijana wa Dar es
Salaam walikuwa na desturi ya kukutana viwanja wa jangwani kufanya
mazoezi na baada ya muda wakaamua kuunda timu yao, waliyoipachika jina
Jangwani Boys.
Ndani ya kipindi kifupi timu hiyo iliteka hisia za wengi, waliojitokeza
kujiandikisha uanachama wa klabu hiyo, miongoni mwao waliovutiwa na
uanachama wa klabu hiyo ni Tabu Mangala (Sasa marehemu) na ilipofika
mwaka 1926 walifanya mkutano wa kwanza katika eneo ambalo hivi sasa kuna
shule ya sekondari ya Tambaza.
Miongoni mwa yaliyojadiliwa kwenye mkutano huo ni kuiboresha timu hiyo
ambayo wachezaji wake wengi walikuwa wafanyakazi wa bandarini na
mashabiki wake wengi walikuwa wabeba mizigo bandarini.
Baada ya mkutano huo, timu ilibadilishwa jina na kuwa Navigation,
iliyotokea kuwa moto wa kuotea mbali katika timu za waafrika enzi hizo,
kabla ya uhuru wa Tanganyika.
Timu kama Kisutu, Kitumbini, Gerezani na Mtendeni zilikuwa hazifui dafu kwa wana wa Jangwani hao.
Enzi hizo kikosi cha Yanga cha ushindani kikiwa uwanjani tayari kwa mchezo
Ikiwa inatamba kwa jina la Navigation, wanachama wa timu hiyo walikuwa
wanatembea kifua mbele na kuwatambia wapinzani wao, kwamba katika
kipindi hicho wao ndiyo zaidi, kwa sababu Italia ilikuwa inatamba kwenye
ulimwengu wa soka, wanachama wa timu hiyo nao waliamua kuibadilisha
jina timu yao na kuiita Italiana.
Taliana FC ilipata mafanikio ya halaka na haikushangaza ilipopanda ligi Daraja la pili kanda ya Dar es Salaam.
Mwanzoni mwa miaka ya 1930 Taliana waliamua kuachana nalo mapema kabla
ya kuingia kwenye ligi hiyo, hivyo wakaanza kujiita New Youngs.
Kila kila ilipokuwa ikibadilisha jina, ilikuwa ikifanya vitu vipya pia,
kwani wakiwa na jina la New Youngs waliweza kutwaa kombe la Kassum,
lililoshirikisha timu mbalimbali za Dar es Salaam.
Hatimaye ukawadia mwaka mbaya kwa New Youngs 1938 wakati baadhi ya wachezaji walipojitoa na kwenda kuanzisha Sunderland.
Kwa sababu hiyo, waliobaki wakaamua kubadili jina na kuwa Young Africans
jina ambalo mashabiki wake wengi walishindwa kulitamka vizuri hivyo
kujikuta wakisema Yanga.
Miaka ya 80 baadaye leo, ni timu ya kihistoria Tanzania ikiwa inaongoza kutwaa ubingwa wa ligi kuu Tanzania bara kwa mara 25.
Pongezi nyingi ziwaendee wachezaji wote waliopata kuichezea timu hiyo
kuanzia enzi za Jangwani Boys, Navigation, Italiana, New Youngs hadi leo
hii ikijulikana kama Yanga ingawa katika cheti chake cha usajili
inafahamika kama Dar Young Africans.
Mafanikio ya Yanga ndani ya miaka 80 hayakuja hivi hivi bila kuwapongeza
viongozi ambao waliihangaikia timu hiyo inasimama kidete, viongozi wa
enzi hizo hadi leo hii wanastahili pongezi kwa kuiwezesha kutwaa mara
nyingi ubingwa wa nchi.
Wachezaji wa zamani wa Yanga ambao kwa sasa wameunda timu yao ya Yanga veterani
Shukrani nyingine ziwaendee wanachama, wapenzi na mashabiki, bila
kuwasahau waandishi wa habari, bila hamasa zao sidhani kama Yanga
ingeweza kufika hapo ilipo, hiyo ndiiyo historia ya klabu ya Yanga
ambayo ndio iliyozaa Sunderland leo hii ikiitwa Simba SC.
Nania angeijua Simba kama si Yanga, hivyo inajivunia ubora ilionao,
Yanga imetoa viongozi mbalimbali wa soka na serikali mmoja wapo ni rais
wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Jakaya Mrisho Kikwete ambaye mwaka
1976 alipokuwa mwenyekiti wa kamati ya usajili wa klabu hiyo na
kuwezesha usajili wa Shaaban Katwila.
Pia Yanga imetoa rais wa CECAFA Leodegar Tenga, rais wa TFF Jamal
Malinzi, nahodha wa Taifa Stars na Zanzibar Heroes Hadir Haroub
'Cannavaro'na kocha wa timu ya taifa, Taifa Stars Charles Boniface
Mkwasa na wengineo.