Kocha wa Yanga, Hans van der Pluijm, amesema timu yake ina mapungufu makubwa kwenye kiungo, lakini pia inahitaji marekebisho makubwa katika safu ya ulinzi.
Akizungumza na gazeti hili jana, Pluijm alisema ushiriki wa Yanga kwenye Kombe la Kagame la klabu bingwa ya Afrika Mashariki na Kati inayofika kilele kesho imemuonyesha mapungufu ya timu yake hayo ambayo anatakiwa kuyafanyia kazi mara moja.
"Hatukuwa katika ubora kwenye safu ya kiungo na ulinzi, ni mambo ya kiufundi na nimeandaa programu ya kuhakikisha tatizo hili nalitatua kwa wakati," alisema Pluijm.
Katika soka la sasa ni lazima kuwe na uwiano katika timu kuanzia nyuma, katikati mpaka mbele na timu yake kwa kiasi fulani ilikosa uwiano ulio sawa, alisema.
"Ukiangalia katika mchezo wetu na Azam ni mambo hayo ndiyo yalitugharimu, hatukucheza vizuri katikati na pia katika mchezo wetu wa kwanza dhidi Gor Mahia utaona safu yetu ya ulinzi pia haikuwa sawa, ni mambo ambayo nayafanyia kazi kwa haraka," alisema Pluijm.
Alisema kuwa baada ya kuondolewa kwenye michuano hiyo ya Kagame, anaendelea na mikakati yake ya kuiandaa timu kwa ajili ya ligi kuu ya Bara na mpaka kufika Septemba 12, siku ya ufunguzi, Yanga itakuwa katika kiwango sahihi.
Licha ya kuondolewa kwenye Kagame katika hatua tya robo-fainali, kocha huyo amepata faida kubwa ya kujua mapungufu ya timu yake na kupata sehemu ya kuanzia kuelekea kwenye mchezo wa Ngao ya Hisani dhidi ya Azam wa Agosti 22, alisema.
Pluijm alisema marekebisho anayokusudia kufanya hayahitaji kusajili mchezaji mpya, hata hivyo, kwa kuwa anachotakiwa kufanya ni kujenga muunganiko mzuri katika timu yake.
"Yupo Salum Telela, yupo Makapu kuna Niyonzima na wengine, wote wana uwezo mkubwa," alisema. "Ni kuwapa mbinu na jinsi ya kuimarisha nafasi hizo."
Yanga inajiandaa kwenda kuweka kambi mkoani Mbeya ambako itacheza mechi tatu za kirafiki kabla ya kurudi jijini kuikabili Azam kwenye Ngao ya Jamii.