Timu ya wanawake ya Japan wakishangilia ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya England katika mchezo wa nusu fainali za Kombe la Dunia nchini Canada.
Mabingwa watetezi wa Kombe la Dunia kwa wanawake, Japan, wameonyesha dhamira ya kulitwaa tena kombe hilo baada ya kuibwaga England kwa mabao 2-1 katika nusu fainali ya pili katika michuano hiyo inayoendelea nchini Canada.
England ambayo katika mashindano hayo ilionyesha kiwango cha juu cha uchezaji hadi kufika nusu fainali imesononeshwa na matokeo hayo baada ya mchezaji wake Laura Bassett kujifunga mwenyewe katika dakika za nyongeza kipindi cha pili.
Timu ya kina dada wa England ilikuwa ikijaribu kuandika historia kwa kutinga fainali kwa mara ya kwanza na pia kuwa fainali ya pili kwa timu za Uingereza, baada ya wanaume kutwaa kombe la dunia mwaka 1966, michuano iliyokuwa imeandaliwa nchini Uingereza.
Hadi kipindi cha kwanza kinamalizika Japan na England zilifungana bao 1-1 yote yakiwa yamepatikana kwa njia ya penalti.
Japan ilikuwa ya kwanza kupata bao katika dakika ya 32 likifungwa na Aya Miyama kwa njia ya penalti. Nao England wakasawazisha katika dakika ya 40 kwa njia hiyo hiyo ya penalti likifungwa na Fara Williams.
Japan ilimiliki mchezo huo kwa asilimia 62, huku England ikiwa na asilimia 32.
Sasa Japan itavaana na Marekani katika mchezo wa fainali siku ya Jumapili.
Kufika fainali Marekani iliitoa Ujerumani kwa mabao 2-0.
Sasa England itapepetana na Ujerumani kumsaka mshindi wa tatu, siku ya Jumamosi.Kiko