Kikosi cha mabingwa watetezi wa Ligi Kuu ya soka Tanzania Bara, Yanga kimewasili salama mkoani Tanga kikiwa bila ya wachezaji wake wawili nyota ambao ni Waganda, Emmanuel Okwi na Hamis Kiiza, imeelezwa.
Yanga iliyokuwa imeweka kambi jijini Antalya, Uturuki iliwasili jana Tanga tayari kuvaana na wenyeji wao Coastal Union ambao walikuwa Muscat, Oman katika mechi ya raundi ya 15 ya Ligi Kuu ya Tanzania Bara itakayopigwa kesho kwenye Uwanja wa Mkwakwani.
Akizungumza jana, Afisa Habari wa Yanga, Baraka Kizuguto, alisema kikosi chao cha wachezaji 20 kilitua salama Tanga tangu jana saa sita mchana na jioni walitarajia kuanza mazoezi kwenye Uwanja wa Mkwakwani ili kujiandaa na mchezo huo wa kesho.
Kizuguto aliwataja baadhi ya wachezaji waliobaki jijini Dar es Salaam kwa sababu tofauti kuwa ni pamoja na Shaaban Kondo, Ibrahim Job, Salum Telela, Hassan Dilunga na Lusajo.
"Tunamshukuru Mungu tumefika Tanga salama, ila tumesafiri na wachezaji 20 na 12 wamebaki Dar es Salaam, mwalimu ndiye anayechagua nani aende na nani abaki kulingana na umuhimu wa mechi husika," alisema Kizuguto.
Aliwaja makipa wote watatu wa timu hiyo ambao ni Juma Kaseja, Deogratius Munishi 'Dida' na Ally Mustaph 'Barthez' kuwa wametua nao jijini Tanga wakiwamo 18 waliokuwa kwenye orodha ya mchezo wao wa kwanza wa mzunguko wa pili walioshinda 2-1 dhidi ya Ashanti United kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam Jumamosi.
Mbali na makipa hao nyota wengine wa Yanga walioko Tanga ni pamoja, Oscar Joshua, Mbuyu Twite, Kelvin Yondani, Frank Domayo, Mrisho Ngasa, Haruna Niyonzima ‘Fabregas’, Said Bahanunzi na David Luhende.
Wengine ni Simon Msuva, Hussein Javu na Didier Kavumbagu.
Taarifa kutoka ndani ya uongozi wa klabu hiyo ya Jangwani zimeeleza kuwa baadhi ya viongozi wa Yanga wataifuata timu leo jijini humo kwa ajili ya kuongeza nguvu kusaka ushindi katika mchezo huo mgumu.
Kizuguto aliongeza kuwa uongozi umemuachia madaraka Kocha Mkuu, Hans van der Pluijm kuchagua wachezaji wa kusafiri kulingana na mahitaji yake.
"Kiiza na Dilunga ni wagonjwa," kilisema chanzo chetu huku wengine wakiachwa kutokana na maamuzi ya kocha mkuu.
Yanga itashuka dimbani kesho ikiwa na kumbukumbu ya kutoka sare ya bao 1-1 kwenye mechi ya mzunguko wa kwanza jijini Dar es Salaam, huku ikijiamini zaidi baada ya Jumamosi kuanza mzunguko wa pili kwa ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Ashanti United ya jijini, wakati Coastal Union yenyewe ililazimishwa sare ya 1-1 na 'Maafande' wa JKT Oljoro kutoka Arusha.
Yanga na Coastal Union zote zitakutana zikiwa na makocha wapya ambao hawakuwapo katika mzunguko wa kwanza wa ligi hiyo inayotarajiwa kumalizika Aprili 27, mwaka huu.